Wanafunzi UDSM waagwa, Kikwete atuma salamu

Waombolezaji wakipita mbele ya miili ya wafanyakazi na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati wa ibada ya kutoa heshima za mwisho, iliyofanyika katika ukumbi wa Nkrumah wa chuo hicho leo. Marehemu hao walipata ajali hivi karibuni jijini Dar es Salaam baada ya gari la wagonjwa na lori kugongana. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Rais mstaafu wa awamu ya nne na Mkuu wa Chuo hicho Jakaya Kikwete alituma salamu za pole na rambirambi kwa njia ya barua

Dar es Salaam. Familia, ndugu na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wametoa heshima zao za mwisho kwa miili ya watu wanne wakiwamo wanafunzi wawili wa chuo hicho, waliofariki katika ajali ya gari Juni 11.

Hata hivyo, Rais mstaafu wa awamu ya nne na Mkuu wa Chuo hicho Jakaya Kikwete alituma salamu za pole na rambirambi kwa njia ya barua baada ya kushindwa kuhudhuria katika hafla ya kuaga miili hiyo kutokana na kuwa nje ya nchi kikazi.

Katika ajali hiyo wanafunzi wawili, Mary Soko na Erasto Stephen, Dereva wa gari hiyo James Rutayuge pamoja na muuguzi msaidizi Jonathan Lung’ando walipoteza maisha papo hapo baada ya gari la wagonjwa walimopanda, kuligonga lori, eneo la Riverside, Ubungo.

 Naibu Makamu Mkuu wa Chuo na Utawala (UDSM) Profesa David Mfinanga  alisoma salamu za Kikwete mbele ya waombolezaji hao.

 “Nimepokea kwa mshtuko, masikitiko na huzuniko taarifa ya vifo vya wenzetu wanne ni msiba mkubwa sana kwa chuo chetu na kwangu na kwa familia za marehemu,”imesema barua ya Kikwete

“Nilitamani sana kuwepo pamoja nanyi katika kipindi hiki kigumu bahati mbaya sitaweza kuwa nanyi kwa sababu niko safarini Havard University kwa shughuli ambazo pia zina maslahi kwa chuo chetu.”

“Naomba unifikishie salamu za rambirambi kwa jumuiya ya chuo kikuu chetu mashughuli na familia za marehemu bwana ametoa na bwana ametwaa jina lake lihimidiwe,” amesema Dk Kikwete.

Mbali na Rais Mstaafu Kikwete kutuma salamu hizo Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi,  Joyce Ndalichako pia ametuma salamu zake ambazo pia zilisomwa na Makamu mkuu wa chuo kutokana na kushindwa kuhudhuria katika hafla hiyo

“Nilitamani sana kujumuika nanyi leo lakini imenibidi kuhudhuria kikao cha bajeti bungeni kinachofanyika mjini Dodoma, naomba sana mpokee salamu zangu za pole,” taarifa ya Ndalichako inaeleza.

Mfinanga amesema kama chuo kimepoteza watu muhimu ambao walikuwa na ndoto za kufanya jambo kubwa katika familia ya chuo cha UDSM.

“Naamini kuwa hata wao huko waliko wanatamani  tufikie kule walikokutaka  japo kama binadamu hawako hapa kucheka nasi wala kutujali bali tunafarijika kwa sababu tunajua huko waliko kuna amani,” amesema Profesa Mfinanga.

Amesema ni ngumu kuelewa kilichotokea na ni ngumu kutambua kilichotokea ila hakuna ajuaye mipango ya Mwenyezi Mungu.

Mwili wa mwanafunzi Erasto Stephen unazikwa leo katika makaburi ya Yombo Vituka na Dereva James Kagwebe unatarajiwa kuzikwa leo maeneo ya Bunju B.

Huku Mwili wa Muuguzi Jonathan Lung’ano ukisafirishwa kuelekea Kaliua, Tabora kwa ajili ya mazishi, kesho na mwili wa Mary Soko unatarajia kuzikwa Ununio, jijini hapa.