Wanafunzi Jangwani wajibebesha lawama matokeo mabaya kidato cha sita lakini...

Wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Jagwani ya jijini Dar es Salaam wakitoka shuleni hapo jana. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Hata hivyo, wamewatupia lawama walimu wao kwa kutohudhuria vipindi.

Dar es Salaam. Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Jangwani wamejibebesha mzigo wa lawama baada ya shule hiyo kushika nafasi ya 451 kati ya 453 katika matokeo ya kidato cha sita yaliyotolewa Julai 13 wakisema, chanzo ni utovu wa nidhamu wa hali ya juu.
Hata hivyo, wamewatupia lawama walimu wao kwa kutohudhuria vipindi.
Wakizungumza na mwandishi wetu jana, wanafunzi hao wamesema tatizo kubwa lililochagiza matokeo hayo ni utovu wa nidhamu uliopitiliza kwa baadhi yao, kutokuwapo kwa adhabu kama ya viboko, umbali wa kwenda na kurudi shule lakini pia baadhi ya walimu kutohudhuria vipindi.
Wameeleza hayo siku chache baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo kuitembelea na kuagiza kufanyika kwa mabadiliko ya walimu.
“Fanyeni mabadiliko ya walimu hawa, haiwezekani mwalimu mmoja akakaa miaka mitano bila kuhamishwa kituo cha kazi,” alisema  Jafo.
Mmoja kati ya walimu shuleni hapo (jina lake linahifadhiwa) alisema nidhamu ya wanafunzi inaporomoka kutokana na Serikali kuzuia adhabu ya viboko kwa wanafunzi.
Alisema baada ya kupiga marufuku ya viboko, walimu wengi shuleni hapo walikuwa wakilalamika lakini hakukuwa na hatua zozote licha ya kutakiwa kutoa adhabu ndogondogo ikiwamo kuchimba mashimo.
Alidai kwamba baadhi ya wanafunzi walikuwa wakijihusisha kimapenzi na walimu huku wengine wakimiliki simu za mkononi kinyume na taratibu za shule.
“Mwaka huu, kuna walimu wawili wa kiume wamefukuzwa shule baada ya kubainika kujihusisha kimapenzi na wanafunzi, kwa mazingira haya mwanafunzi hawezi kufaulu lakini tunashukuru tatizo hili limeanza kupungua kwa sasa,”alisema.
Mwanafunzi wa kidato cha pili Anna Mary Macha, alisema sababu za kufeli ni tabia mbaya za wanafunzi.
“Mara kadhaa baadhi ya hao waliomaliza shule, nilikuwa nikiwaona wakiwa wanavaa nguo fupi, na tabia hizo zilikemewa na walimu lakini sikuona mabadiliko, adhabu walikuwa wanapewa waliokuwa against (kinyume),” alisema Anna aliyekuwa akizungumza huku akiwa na urembo katika meno yake. 
Mwanafunzi wa kidato cha tatu, Ritha Mabula alisema tatizo lililojitokeza ni walimu kutowekeza nguvu zaidi kwa wanafunzi hao wakidhani kuwa wamemaliza shule.
“Nguvu inatumika zaidi  huku kwetu ndiyo maana unashangaa matokeo ya ‘O Level’ yanakuwa makubwa, huku tunafaulu sana kuliko ‘A level’,” alisema.
Alisema kuondolewa kwa adhabu ya viboko pia kumechagiza kuporomoka kwa maadili.
“Baada ya kuondoka kwa Mwalimu Manyilizu, ‘discipline’ (nidhamu) ya wanafunzi ikaendelea kushuka zaidi kwani alikuwa akiogopwa sana,” alisema.
Mmoja kati ya wanafunzi waliohitimu kidato cha sita kwa masomo ya Sayansi, Shuwenga Saleh alisema tatizo ni umbali:
“Unatoka shuleni saa kumi na moja jioni unafika nyumbani Mbagala saa mbili usiku, ukifika nyumbani kazi nyingine, muda ni kidogo kwa wanafunzi kujisomea, ndio maana mimi familia yangu wakanitafutia hosteli jirani na shule,” alisema Shuwenga.
Mkuu wa Shule hiyo, Geradine Mwaisenga hakuwapo shuleni hapo na alipotafutwa kwa simu alisema  yupo kwenye kikao cha walimu, ofisa elimu Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Mbando.