Wanafunzi shule ya msingi wabuni taulo ya kike

Muktasari:

  • Mwanaidi anasema watoto wanapoingia katika hedhi kijijini kwao wengi wao hulazimika kubaki nyumbani kwa kuhofia kuchafuka na kuaibika mbele za watu.

Mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Chikopelo Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma, Mwanaidi Yakobo ni miongoni mwa mamia ya wanafunzi wasichana nchini wanaopitia changamoto za kukosa masomo wakati wanapoingia katika hedhi kutokana na kutomudu gharama za bei za taulo za kike.

Mwanaidi anasema watoto wanapoingia katika hedhi kijijini kwao wengi wao hulazimika kubaki nyumbani kwa kuhofia kuchafuka na kuaibika mbele za watu.

“Wazazi wangu walikuwa wananiambia nibaki nyumbani hadi nimalize hedhi, hali iliyokuwa ikinilazimu kukaa nyumbani kwa kati ya siku nne hadi tano kila mwezi,” anasema.

Anasema ili kujihifadhi alikuwa akitumia nguo chakavu ambazo baada ya kutumika huzifua na kisha kuzianika chini ya godoro kuzuia watu kuziona.

Lakini baada ya kuanzishwa klabu shuleni kwake, mwalimu wake wa afya aliwafundisha namna ya kutengeneza taulo (pads) za asili kwa gharama nafuu.

“Baada ya kuipata elimu hii nilienda kuwafundisha pia wenzangu nyumbani na sasa tunatengeneza na kutumia wote, sijawahi tena kukosa shule kwasababu hii,” anasema Mwanaidi ambaye alikuwa anatoa ushuhuda wa ubora na faida za taulo hizo katika warsha iliyoandaliwa na Mradi wa Usafi wa Mazingira (Umata)

INAENDELEA UK24

Inatoka Uk23

unaoendeshwa na Shirika la Plan International Tanzania.

Mwalimu wake Rachel Chamhene anasema walianzisha klabu hiyo mwaka 2015 baada ya kupata elimu juu ya utengenezaji wa taulo hizo kutoka Umata.

Anasema wanafunzi wanaohusika kufundishwa namna ya kutengeneza taulo hizo ni wale wa darasa la tano na la sita na utaratibu huo umekuwa hivyo ili kutoa muda kwa darasa la saba kuendelea na maandalizi ya mitihani ya kumaliza elimu ya msingi.

Utengenezaji wa taulo

Rachel anasema vifaa vya kutengenezaji taulo hizo ni vya gharama ndogo na kwamba wanatumia ngozi, kitambaa cha pamba, pamba yenyewe, nailoni, uzi, sindano, mkasi ama wembe katika matayarisho ya taulo hizo.

Anasema pamba na gozi ndio hutupwa baada ya kutumika huku kitambaa na nailoni vikiendelea kuhifadhiwa na kutumika kwa muda mrefu kwasababu si rahisi kuharibika.

“Unaweza ukatumia nailoni na kitambaa kwa muda mrefu sana na endapo kitapata uchafu kidogo wakati wa matumizi basi unakifua na kisha kukianika hadi kikauke vizuri na kukihifadhi kwa ajili ya kutengeneza taulo nyingine wakati mwingine,” anasema.

Anasema pia wanachumba maalumu kwa ajili ya kubadilishia taulo kwa wasichana wanapokuwa katika hedhi ambapo huwekwa taulo zilizotengenezwa na wanafunzi na kifaa cha kuhifadhia zilizotumika.

Rachel anasema tangu waanze mafunzo hayo, wamesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza utoro kwa wanafunzi wa kike uliokuwa ukitokana na kukosa vifaa vya kujifadhia wanapokuwa katika hedhi.

Alitoa mfano wa darasa moja wakati bado hawajaanza utengenezaji wa taulo za asili lenye wanafunzi wakike 12, wanafunzi wanne walikosa masomo kwasababu ya kukosa taulo za asili.

“Kupitia mikutano ya wazazi tulielimisha kuhusu mradi huo ili wachangie katika kuwasaidia watoto wa kike waweze kuhudhuria masomo yao ipasavyo bila kukosa kwasababu ya taulo,” anasema.

Chimbuko la taulo

Mratibu wa Programu ya Umata wa Shirika la kimataifa la Plan na mwezeshaji wa masuala ya hedhi, Rahel Stephen anasema mradi huo wa usafi shuleni ni sehemu ya mradi wa Umata ambao upo katika wilaya tatu za Kongwa, Bahi na Chamwino.

Anasema mradi huo wa usafi shuleni unaangalia pia upatikanaji wa taulo za kike na sehemu ya kujihifadhia kwa wanafunzi wa kike na kwamba ulianza mwaka 2015 Wilaya ya Bahi.

Rahel anasema walianza kwa kutoa mafunzo kwa walimu na walezi wa klabu za afya shuleni kwa kuwajengea uwezo wa kuwasaidia wanafunzi wa kike teknolojia rahisi ya utengenezaji wa taulo hizo.

“Miongoni mwa shule za msingi ambazo zimeanza kutengeneza (taulo hizo) ni hiyo ya Chikopelo. Wanafunzi walikuwa wakitumia vitambaa vilivyochakaa (wakiwa katika hedhi) ambavyo vinalowana mapema. Lakini sasa baada ya kuwafundisha teknolojia rahisi ambayo material (malighafi) hupatikana kirahisi sasa wameanza kutengeneza na kuzitumia,” anasema.

Anasema baada ya wanafunzi kuipata elimu hiyo wamekuwa wakirudi nyumbani na kuisambaza kwa wengine.

Anasema mwiitikio umekuwa mkubwa baada ya kutoa elimu kwa klabu, walezi wa klabu hizo katika shule za sekondari na msingi na waratibu wa afya.

Rahel anasema baadhi ya shule zimeanza kutenga fedha kwa ajili ya kununua taulo za dukani ili mwanafunzi anapopatwa na dharura shuleni basi ajisitiri badala ya kurudi nyumbani na kukosa masomo.

“Changamoto bado ipo kuna baadhi ya walimu hasa wanaume wanaliona kuwa hilo ni jambo dogo tu hivyo hawatengi fedha kwa ajili ya taulo za kike, lakini kwetu hata kama ni mwanafunzi mmoja anakosa masomo kwasababu hiyo tunaliona ni tatizo,” anasema.

Hata hivyo, anasema wanahamasisha kuwepo kwa shule juu ya kutenga fedha kwa ajili ya taulo za kike ili kuwe na mwendelezo wa suala hilo.

“Nasema hivyo kwasababu kama sasa walimu wa Shule ya Chikopelo wanatenga fedha kwa ajili ya jambo hili huwezi kujua watakaokuja baada ya hawa kama watafanya hivi,” anasema.

Mganga mkuu alonga

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk James Charles anasema taulo hizo ni salama ukilinganisha na vifaa vingine vya asili wanavyotumia wanawake wengi wa vijijini kwawsababu vinatengenezwa katika mazingira ya usafi.

Anasema athari ya kutumia vifaa vya kujihifadhia wakati wa hedhi visivyo visafi ni pamoja na mtumiaji kupata maambukizo yasiyoisha na baadaye madhara katika njia ya haja ndogo na uzazi.

“Mtu anayetumia vifaa visivyo visafi anaweza pia akapata michubuko au majipu kwasababu ya joto,” anasema Dk Charles.

Kuna umuhimu wa kuwepo bajeti maalumu kwa ajili ya kuwasaidia watoto wa kike nchini. Umuhimu huo hauzungumzwi na mashirika yasiyo ya kiserikali pekee, bali hata baadhi ya wabunge wamekuwa wakipaza sauti zao kuitaka Serikali kuona umuhimu wa kutenga bajeti maalumu kwa ajili ya wanafunzi hawa na kuondoa kodi kwenye taulo za kike ili kupunguza gharama za kununua.

Mbunge wa Viti Maalum, Upendo Peneza wakati akichangia bajeti kuu ya Serikali mwaka 2017/18 anasema kwa kuweka mfumo huo utawawezesha wanawake kushiriki vyema katika shughuli za uchumi kama wanaume.