Wanafunzi wa St Joseph wadai kulipwa Sh6 bilioni

Muktasari:

Katika kesi hiyo iliyopangwa kuanza kusikilizwa Septemba 13 na Jaji Winfrida Koroso, wanafunzi wanne Ramadhan Kipenya, Innocent Peter, Faith Kyando na Mohammed Mtunguja waliruhusiwa kuwawakilisha wenzao mahakamani hapo.

Dar es Salaam. Wanafunzi 316 waliokuwa wakisoma katika Chuo Kikuu cha St Joseph waliorudishwa nyumbani kwa kukosa sifa, wamefungua kesi ya madai ya Sh6 bilioni kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam dhidi ya chuo hicho na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).

Katika kesi hiyo iliyopangwa kuanza kusikilizwa Septemba 13 na Jaji Winfrida Koroso, wanafunzi wanne Ramadhan Kipenya, Innocent Peter, Faith Kyando na Mohammed Mtunguja waliruhusiwa kuwawakilisha wenzao mahakamani hapo.

Wanafunzi hao ambao wanatetewa na Wakili, Emmanuel Muga wanaiomba mahakama iamuru walipwe zaidi ya Sh1 bilioni kama gharama  ikiwamo za ada walizokilipa chuo hicho.

Pia, wanaomba kulipwa Sh5 bilioni kama fidia ya jumla ya gharama za  hasara  walizozipata.

Wakili Muga ambaye anawawakilisha wanafunzi hao aliiomba Mahakama kuendesha kesi hiyo kwa haraka, kwa sababu wanafunzi hao wapo mtaani na hawajui hatima yao huku fedha zao zikiwa zimeliwa.

Chuo Kikuu cha St. Joseph katika kesi hiyo kinawakilishwa na Wakili Jerome Msemwa, huku TCU ikiwakilishwa na Wakili Rose Rutta.