Wanafunzi wa shule ya msingi wakutwa na misokoto 59 ya bangi

Moshi. Watu wawili wamefariki dunia katika matukio mawili  tofauti huku jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro linawashikilia wanafunzi wa Shule ya Msingi Msamadi iliyopo wilayani Hai kwa kukatatwa na bangi misokoto 59.

Kamanda wa polisi mkoani hapa, Hamisi Issah alisema Mei 28, mwaka huu, majira ya saa 10:30 Kijiji cha Kyengia wilayani Siha mwananmke mmoja Ephrata Masaki(53), alipigwa na shoti ya umeme wakati akianua nguo.

Alisema nguo hizo zilikuwa zimeanikwa kwenye waya uliokuwa umegusana na waya wa umeme nyumbani kwake na kwamba waya huo ulikuwa umechubuka na kusababisha kifo chake.

Alisema Mei 28, mwaka huu, majira ya saa 12:00 jioni, Kata ya Soweto mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Sadia Kamote(39), mkazi wa Sanya juu, aligundua kufariki kwa mtoto wake wa darasa la kwanza.

Alisema mwanafunzi huyo aliyejulikana kwa jina la Selemani Said(8) ni wa Shule ya Msingi Kilingi alifariki baada ya kuteleza kutoka kwenye jiwe na kusombwa na maji katika mto Karanga katika daraja la Mangia Shirimatunda.

“Mwanafunzi huyo alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu huku wenzake aliokuwa akiogelea nao katika mto huo wenzake watatu kunusulika kifo,”alisema Kamanda Issah.

Alisema mwili wa marehemu Masaki umehifadhiwa katika hospitali ya Kibong’oto kwa taratibu za mazishi huku mwili wa mtoto huyo umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mawenzi.

Katika tukio lingine  Mei 28, mwaka huu, majira ya saa 10:30 katika kijiji cha kwa Sadala jeshi hilo liliwakamata wanafunzi wanne wakiwa na begi dogo jeusi na baada ya kuwapekuwa walikutwa na bangi.

“Tulipowahoji watoto hao walisema walipewa mzigo huo na mama aliyejulikana kwa jina la Francisca Limo(43) kwa lengo la kwenda kuuza na tayari tumeshawakamata watuhumiwa kwa mahojiano zaidi,”Kamanda Issah.