Wanafunzi wagoma kutumia maji yaliyowekewa dawa

Muktasari:

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Anthony Mayo alisema jana kuwa kutoakana na hatua hiyo, wanafunzi wako katika hatari ya kupata magonjwa ya tumbo.

Morogoro. Wazazi wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Kiziwa wilayani Morogoro wanadaiwa kuukataza uongozi wa shule hiyo kuweka dawa kwenye maji ya kisima ili kuyatibu.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Anthony Mayo alisema jana kuwa kutoakana na hatua hiyo, wanafunzi wako katika hatari ya kupata magonjwa ya tumbo.

 “Hata tulipoletewa dawa za minyoo na matende haikuwa rahisi kuwapatia wanafunzi, walikuwa hawataki kumeza kwa kutumia maji ya hapa shule,” alisema Mwalimu Mayo.

Mwanafunzi wa darasa la saba, Salma Sadick alisema kipindi cha nyuma wanafunzi walisumbuliwa na ugonjwa wa kichocho lakini Serikali kwa kushirikiana na mashirika mengine waliamua  kugawa dawa za kutibu maji ambazo wazazi wao wanadai kuwa zina madhara.