Sunday, October 22, 2017

Wanafunzi watishia kuchoma shule moto

By Rehema Matowo, rmatowo@mwananchi.co.tz

Vurugu zimeibuka katika Shule ya Sekondari Geita (Geseco) baada ya wanafunzi 509 wa kidato cha tano na sita kutishia kuchoma shule wakishinikiza wenzao wanne wanaoshikiliwa na polisi waachiwe huru.

Vurugu hizo zilizoanza juzi saa moja usiku kwa wanafunzi kurusha mawe juu ya bati kuzuia kikao cha bodi ya shule kuendelea zimesababisha wanafunzi hao kurudishwa nyumbani hadi Novemba 24 mwaka huu.

Mkuu wa shule hiyo, Isaya Busagwe alisema kamati ya shule imeridhia wanafunzi hao warudi nyumbani na baadae watalazimika kuja na wazazi wakiwa na barua ya mwenyekiti na mtendaji wa kijiji.

Akizungumzia chanzo cha vurugu hizo, Busagwe alisema Oktoba 14 mwaka huu wanafunzi wanne wa kidato cha sita, usiku walimwita mwanafunzi wa kidato cha tano kisha kumpiga na kumjeruhi mgongoni. “Hatukujua mapema ilipofika Jumatatu mwanafunzi aliyepigwa aliomba ruhusa ya kurudi nyumbani, alipohojiwa sababu za kutaka kwenda nyumbani ndiyo akasema anaumwa mwalimu alivyomdadisi akaonyesha alivyopigwa na wenzie.

“Tulimpeleka polisi akapewa PF3 na baadae hospitali, kwenye kundi la watu waliompiga aliwatambua wanne na kuwataja,” alisema Busagwe.

Mkuu huyo alisema bodi ya shule ilikutana saa moja usiku kutafuta muafaka lakini wanafunzi walianza kurusha mawe juu ya bati huku wakitishia kuchoma majengo moto.

“Tulivyoona hali inazidi kuwa mbaya maana walisogea hadi kwenye nyumba za walimu tulipiga simu polisi,” alisema.

Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo, Eliangikaya Mshana alisema kamati imeamua wanafunzi hao warudi nyumbani kupisha wenzao wa kidato cha pili na cha nne wanaojiandaa na mitihani kufanya mitihani yao bila usumbufu.

“Hii shule kidato cha kwanza hadi cha nne ni mchanganyiko na ni wakutwa lakini kidato cha tano na sita ni wa bweni na ndiyo sababu tumewatoa warudi nyumbani hadi mitihani itakapoisha ndiyo warudi na wazazi wao,”alisema Mshana

Wanafunzi Vedastus Marwa na Nicodemas Yohana wa kidato cha tano ambao walikimbia na kulazimika kulala kanisani walisema ili waishi kwa amani shuleni hapo wanalazimika kusikiliza uamuzi wa wanafunzi wa kidato cha sita.

-->