Wanahabari wapinga sheria kortini

Muktasari:

Katika kesi hiyo, namba 2/2017 iliyofunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, wadai hao wanaowakilishwa na jopo la mawakili sita wakiongozwa na Wakili Fulgance Massawe wanadai sheria hiyo iliyopitishwa Novemba 5, mwaka jana inakiuka Ibara ya 18 ya Katiba.

Mwanza. Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), kwa kushirikiana na Kampuni ya Hali Halisi Publishers Limited, jana walifungua kesi ya kikatiba kupinga baadhi ya vifungu vya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 wakidai vinakiuka Katiba na kuminya uhuru wa maoni.

Katika kesi hiyo, namba 2/2017 iliyofunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, wadai hao wanaowakilishwa na jopo la mawakili sita wakiongozwa na Wakili Fulgance Massawe wanadai sheria hiyo iliyopitishwa Novemba 5, mwaka jana inakiuka Ibara ya 18 ya Katiba.

Wamesema vifungu vinavyokiuka Katiba ni vile vinavyominya uhuru wa maoni na uhuru wa vyombo vya habari.

Mawakili wengine katika shauri hilo ni Edwin Hans, Mpale Mpoki, Jenerali Ulimwengu, Jebra Kambole na Francis Stolla.