Wanaharakati wakwama mahakamani sakata la wanafunzi wajawazito kuondolewa shuleni

Takwimu za 2007 zinaonyesha Mkoa wa Mtwara uliongoza kwa wanafunzi 435 kuacha shule kutokana na ujauzito.

Muktasari:

DONDOO

  • Takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi zinaonyesha tangu 2004 hadi 2008, wastani wa wanafunzi wa kike 5,720 nchini wanaacha shule kila mwaka kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo ujauzito.
  • Takwimu za 2007 zinaonyesha Mkoa wa Mtwara uliongoza kwa wanafunzi 435 kuacha shule kutokana na ujauzito. 
  • Mikoa iliyofuata na idadi ya wanafunzi waliopata ujauzito katika mabano ni Mwanza (308), Tanga (290), Pwani (280), Rukwa (265), Ruvuma (204), Lindi (144), Shinyanga (137), Dodoma (111) na Mbeya (105).

Dar es Salaam. Jitihada za wanaharakati kutetea wanafunzi wanaopata ujauzito wakiwa shuleni kuendelea na masomo baada ya kujifungua zimegonga mwamba kutokana na Mahakama Kuu kukubaliana na Kanuni za Elimu za mwaka 2002, zinazozuia wanafunzi hao kuendelea na masomo.

Uamuzi huo wa Mahakama Kuu umekuja siku chache baada ya kuwepo kwa mvutano wa kauli baina ya wanaharakati na wadau wengine wa elimu nchini na Rais John Magufuli, kuhusu wanafunzi hao kuendelea na masomo baada ya kujifungua.

Mwezi Juni mwaka huu, Rais Magufuli alitoa msimamo kuwa ni marufuku kwa wanafunzi wanaopata mimba kurudi shuleni, hasa katika shule za umma kama ambavyo Kanuni za Elimu za mwaka 2002 zinavyoelekeza.

Msisitizo wake huo uliibua mjadala miongoni mwa wanaharakati na wadau wa elimu, wakimpinga na baadhi wakimuunga mkono.

Hata hivyo, Mahakama Kuu imekazia msimamo huo wa Rais Magufuli ambao pia ni msimamo wa kisheria, baada ya kulitupa shauri lililofunguliwa na mashirika ya wanaharakati wa haki za binadamu kuhusiana na  suala hilo.

Shauri hilo la Maombi Anuai ya Kikatiba ya 2012, lilifunguliwa na Shirika la Kitaifa la Msaada wa Kisheria (Nola) na Kituo cha Msaada wa Kisheria na Haki za Binadamu (LHRC), mwaka 2012.

Ingawa shauri hilo lilifunguliwa na mashirika hayo dhidi  ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Chama cha Wanasheria Wanawake (Tawla) nacho kiliomba kujumuishwa katika shauri hilo kama mdau mwenye masilahi.

Wanaharakati hao walikuwa wakipinga utekelezaji wa Kanuni za Elimu za mwaka 2002, Tangazo la Serikali (GN) namba 295 la mwaka 2002, hasa kifungu cha 7 (b) (Kutengwa na Kuondolewa shuleni wanafunzi).

Kanuni hiyo ilitungwa na Waziri wa Elimu chini ya kifungu cha 61 (0) cha Sheria ya Elimu (Sura 353 marekebisho ya mwaka 2002).

Walikuwa wakidai kuwa kifungu hicho cha kanuni hizo kimekuwa kikitumiwa na mamlaka za shule kwa kuwalazimisha kuwafanyia vipimo vya ujauzito wanafunzi wa kike na hivyo kuwafukuza shuleni wale wanaobainika kuwa na mimba.

Walikuwa wakidai kuwa kuwalazimisha kuwapima ujauzito kunakiuka haki ya faragha na utu kwa wanafunzi wa kike na kuwafukuza shule wanafunzi hao ni kuwanyima haki ya elimu, na kwamba kanuni hiyo  haiweki usawa kwani haiwahusishi wanafunzi wa kiume na hivyo ni ya kibaguzi.

Hivyo walikuwa wakiiomba mahakama hiyo itamke na kuamuru kuwa kuwapima ujauzito kwa lazima wanafunzi hao kunakiuka haki ya faragha na utu na kwamba kuondolewa shuleni kunawanyima haki ya elimu na ni kinyume na Katiba ya nchi.

Pia, walikuwa wakiiomba mahakama imwamuru Waziri wa Elimu ndani ya miezi mitatu tangu kutolewa kwa amri hiyo kuweka utaratibu na sera ya kuwawezesha wale wote walioathirika na kanuni hiyo kurejea shuleni.

Mahakama katika hukumu yake iliyotolewa na jopo la majaji watatu lililoongozwa na Jaji Kiongozi Ferdinand Wambali, akishirikiana na Jaji Sakieti Kihiyo na Jaji Pellagia Khaday, ilizitupa hoja za wanaharakati hao ikisema kuwa hazina mashiko kwani walishindwa kuthibitisha madai yao.

Akisoma uamuzi huo, Jaji Wambali alisema itakuwa ni jambo lisilowiana ikiwa mamlaka za shule hazitakuwa na mamlaka ya kuwakaripia au kumwadhibu mwanafunzi ambaye kuna tuhuma za msingi kwamba amekiuka sheria au kanuni zinazoratibu taratibu za kawaida za shule.

Alisema wadai hawakuweza kutoa ushahidi kuthibitisha kuwa masharti ya kanuni hiyo si ya kikatiba, wala kuonyesha namna gani yanavyokiuka haki za elimu, faragha na utu wa wanafunzi hao.

Alisisitiza kwamba hapakuwa hata na kielelezo au kiapo kutoka kwa hao wanaodhaniwa kuathirika na tafsiri na matumizi ya kanuni hiyo, yaliyoambatanishwa kwenye shauri lao kama sheria inavyotaka.

Baada ya kurejea kifungu hicho cha kanuni hizo, alisema kuwa masharti yake hayaweki tofauti kati ya msichana na mvulana katika suala la kuondolewa shuleni kutokana na masuala ya kinidhamu.

Licha ya kutambua haki za msingi za binadamu, hata hivyo alisema kuwa  haki hizo zina mpaka.