Wanaharakati washauriwa kuandaa mitalaa kupinga ukatili

Muktasari:

Mitalaa itatumika kuwafundisha watoto namna ya kujilinda tangu wakiwa wadogo.

Dar es Salaam. Wanaharakati wa haki za watoto na wanawake wametakiwa kuandaa mapendekezo kuwezesha kuwapo mitalaa ya kupinga ukatili wa kijinsia.

Imeelezwa mitalaa itasaidia watoto kupewa elimu ya kupambana na suala hilo tangu wakiwa shule za msingi.

Takwimu za ukatili wa kijinsia nchini zinaonyesha kati ya watoto wa kike watatu mmoja ameshafanyiwa ukatili wa kingono; wakati kati ya watoto saba wa kiume, mmoja amefanyiwa ukatili huo.

Akizungumza leo Jumanne Desemba 12,2017 katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia katika viwanja vya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) yakiwahusisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori amesema takwimu za ukatili wa kijinsia zilizopo zinahitaji nguvu ya pamoja kupambana nao.

Makori amesema kwa muda mrefu wanaharakati wamekuwa wakipambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia lakini bado yapo matukio yanayoendelea kutokea kwenye jamii.

Amesema lazima ipatikane dawa ya kupambana nayo, moja wapo ikiwa mitalaa itakayotumika kuwafundisha watoto namna ya kujilinda tangu wakiwa wadogo.

Kaimu Mkurugenzi wa TGNP, Grace Kisetu amesema ukatili wa kijinsia ni vita inayohitaji nguvu ya pamoja kupambana nayo.

Amesema katika maadhimisho ya mwaka huu wamewahusisha wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu kwa sababu ni kundi maalumu linalopaswa kuelewa na kujua namna ya kujikinga wakati wanapokutana na ukatili huo.