Wanamuziki 400 kutumbuiza Sauti za Busara

Picha ya Maktaba

Muktasari:

  • Akizungumza katika mkutano na vyombo vya habari leo, mkurugenzi wa bodi wa tamasha hilo Simai Mohammed alisema katika tamasha hilo kunatarajiwa kuwa na vikundi 20 kutoka Tanzania na 20 kutoka Afrika na kwingineko.

Dar es Salaam. Jumla ya wanamuziki 400 kutoka vikundi 40 wanatarajiwa kutumbuiza katika tamasha la Sauti za Busara linalotarajiwa kuanza kurindima Februari 9-12 mwaka huu, katika viwanja vya Ngome Kongwe visiwani Zanzibar.

Akizungumza katika mkutano na vyombo vya habari leo, mkurugenzi wa bodi wa tamasha hilo Simai Mohammed alisema katika tamasha hilo kunatarajiwa kuwa na vikundi 20 kutoka Tanzania na 20 kutoka Afrika na kwingineko.

"Hili ni tamasha kubwa, hivyo ni vema Serikali ikaweka mkono wake katika kutambua namna linavyovutia watalii, kuingia fedha za kigeni na kwa mwaka huu tumepokea maombi kutoka kwa wasanii 800 lakini tukachagua vikundi 40 pekee," alisema Simai.

Mkurugenzi wa tamasha hilo, Yusuf Mahmoud alisema kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa tamasha, mwaka huu tamasha litakuwa na majukwaa watatu yatakayotumbuiza muziki wa Afrika mfululizo kuanzia saa 10:30 alasiri mpaka saa 7:00 usiku.

Alisema tamasha hilo litaanza kwa gwaride kutoka maeneo ya Kisonge (Karibu na Michenzani) kuanzia saa 9:00 jioni Februari 9 mwaka huu.