Wananchi Mwanza waja na mapya kuhusu usalama wa abiria majini

Muktasari:

  • Maboya hayo ni muhimu katika uokoaji wa abiria pindi ajali zinapotokea.

Mwanza. Baadhi ya wakazi jijini Mwanza wamewalalamikia wafanyakazi wa vivuko na meli nchini kushindwa kugawa maboya ya uokoaji kwa abiria wanaosafiri kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.

Maboya hayo ni muhimu katika uokoaji wa abiria pindi ajali zinapotokea.

Wakizungumzia na Mwananchi kuhusu ajali ya kivuko cha Mv Nyerere mjini hapa, wakazi hao walisema wafanyakazi wa vyombo hivyo hawapo makini katika utekelezaji wa sheria za usalama majini.

Katika mazungumzo hayo, walisema iwapo kivuko hicho kingekuwa na maboya ya kutosha na yakagawiwa mapema kwa wasafiri huenda yangesaidia kupunguza athari na vifo.

Wananchi hao walisema maboya yanayokuwa kwenye vivuko na meli yanapaswa kugawiwa kwa abiria wanapoanza safari.

Hata hivyo, uzoefu wao ni kwamba hukumbukwa ajali ikishatokea na hakuna njia nyingine inayotumika kujinusuru kwa sababu maboya hayo hufungiwa stoo au hufungwa kwa kutumia vyuma au minyororo.

Mkazi wa Ukara aliyehojiwa na Mwananchi jijini hapa, Egda Mugeta alisema sheria inapaswa kutungwa upya huku ikiwekewa kanuni zitakazowabana wafanyakazi wa vyombo hivyo kugawa vifaa vya uokoaji mapema.

“Idadi (ya waliopoteza maisha) haijulikani ya watoto, wanawake, wazee na vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa,” alisema Mugeta.

Mugeta alisema huenda ajali hiyo ilisababishwa na uzembe na hivyo uchunguzi wa kina unapaswa kufanyika.

“Maboya kwenye kivuko hicho yalitakiwa yawe 101 kama idadi ya abiria inayotakiwa na ya dharura walau 21 jumla yalipaswa kuwa 131.”

Selemani Kassim alisema sheria inatakiwa kusisitiza pia kuwa ni lazima kila abiria avae boya shingoni kama inavyokuwa kwa viongozi wa kiserikali wanapoingia kwenye vivuko. “Vilevile tunahitaji elimu kwa abiria wanaotumia usafiri wa majini, mbona kwenye ndege tunaelimishwa namna ya kujiokoa ikitokea dharura?” alisema Kassim.

Mkazi wa Nyamagana, Abdallah Guel alisema unapaswa kuwapo kwa utaratibu mzuri wa wakatisha tiketi kutunza vizuri rekodi zao pamoja na majina ya abiria.

Alisema haoni sababu ya mkatisha tiketi kubeba kitabu cha majina na kupanda nacho kwenye boti, kivuko au meli badala ya kukiacha ofisini ili kama kuna dharura watu waweze kuwatambuliwa kwa urahisi.

“Kwa mfano hapa tunaambiwa majina yameshindwa kupatikana kwa sababu mkatisha tiketi aliondoka nayo, yamezama kwenye maji, si rahisi kutambua ni nani na nani alikuwamo kwenye kivuko hicho, hili jambo walitazame kwa makini,” alisema Guel.

Mama ambaye hakutaka jina lake liandikwe alimpongeza Rais John Magufuli kwa kutangaza siku nne za maombolezo, lakini aliomba ufanyike uchunguzi wa kina wa ubovu wa miundombinu ya vivuko na kuwachunguza watendaji wasiozingatia ushauri na maelekezo ya wataalamu.

Juzi usiku, Rais Magufuli alitangaza siku nne za maombolezo ya kitaifa na pia kuwaahidi Watanzania kuwa Serikali itafanya uchunguzi wa kina ili kuja na majibu yaliyoacha maswali kufuatia ajali hiyo.

Adha ya usafiri

Kutokana na ajali hiyo, hali ya usafiri hadi Ukerewe kwa njia ya Ziwa Victoria jana ilikuwa ngumu kwa sababu ya idadi kubwa ya wasafiri wanaotaka kwenda kisiwani humo kwa ajili ya utambuzi wa miili ya ndugu zao na mazishi.

Hali hiyo imechangiwa na kuwapo kwa kivuko pekee cha Mv Nyehunge ambacho kinafanya kazi kati ya sehemu hizo.

Kutokana na hali hiyo, inaelezwa kuwa sasa baadhi ya watu wanalazimika kupita wilayani Bunda mkoani Mara kwenda eneo la tukio.

Usafiri wa kupitia Bunda ni wa basi na humlazimu abiria kutoka Mwanza hadi Bunda kisha Kisorya kabla ya kufika Nansio yalipo makao makuu ya Wilaya ya Ukerewe.