Wanaobomolewa majengo walipewa notisi- Rahco

Muktasari:

Majengo mawili ya ghorofa, kituo cha mafuta cha Gapco na Soko la Kibasila yalibomolewa eneo la Kamata, Kariakoo jijini hapa jana na juzi yakielezwa kuwa ndani ya hifadhi ya reli.

Dar es Salaam. Ofisa Uhusiano wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (Rahco), Catherine Moshi  amesema waliovunjiwa  nyumba walipewa notisi kwa awamu nne na ya tano ndiyo wanayoitekeleza sasa.

Majengo mawili ya ghorofa, kituo cha mafuta cha Gapco na Soko la Kibasila yalibomolewa eneo la Kamata, Kariakoo jijini hapa jana na juzi yakielezwa kuwa ndani ya hifadhi ya reli.

Bomoabomoa hiyo inayoendeshwa  Rahco, ilianza mwezi huu.

 “Tulishatoa notisi tangu mwaka jana, eneo hili waliweka zuio Julai mwaka jana na kesi ipo mahakamani hivyo tuliacha. Mwanasheria amefuatilia na kutuletea majibu kuwa walipewa muda wa miezi sita ambao umekwisha na hakuna nyingine, hivyo tuendelee na ubomoaji,” amesema.