Wanaodhalilisha watoto wa mitaani kuwekwa hadharani

Muktasari:

Naibu Meya wa Jiji la Mwanza, Bhiku Kotecha amesema Wilaya ya Nyamagana wameshawapeleka baadhi ya watoto shule na wanapata huduma mbalimbali bure

Wakati taasisi mbalimbali zikisaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu kwa kuwaweka pamoja na kuwalea, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amesema anaendelea kufuatilia baadhi ya matajiri wanaowadhalilisha watoto wa mitaani usiku ili kuwatangaza hadharani na kuwachukulia hatua.

Akizungumza wakati wa kikao cha Kamati ya ushauri (RCC) Mkoa wa Mwanza, Mongella alisema tayari ameshapata taarifa ya kuwa wapo baadhi ya watu wenye uwezo wao ambao huutumia kuwadhalilisha watoto hao.

Alisema anaendelea kulitafutia ufumbuzi suala hilo kwa undani na kuhakikisha anawabaini wahusika na kuwatangaza hadharani kabla ya kuchukuliwa hatua.

“Nimepata taarifa kuwa kuna baadhi ya watu wenye uwezo wao, ambao huutumia kuwadhalilisha watoto waishio mitaani hasa usiku,” alisema Mongella.

Awali, wakati akichangia hoja Katibu Mkuu wa Chama cha UDP Mkoa, Edward Mboji alishauri kuwapo operesheni maalumu ya kuwasaka watoto waishio mitaani waliofikisha miaka ya kwenda shule ili kuwapatia elimu.

Mboji alisema kumekuwapo na ongezeko la watoto wa mitaani jijini Mwanza na kwamba bila kuwatafutia mazingira mazuri wataanza kuteka watu na kuvunja nyumba.

“Nishauri pawepo operesheni maalumu ya kuwakamata watoto wote ambao wameshafikisha umri wa kwenda shule na hii iwe ya mkoa kwa ujumla ili kuondoa utitiri wa watoto hao ambao baadaye watatuteka au kutuvunjia nyumba,” alisema Mboji.

Naibu Meya wa Jiji la Mwanza, Bhiku Kotecha alisema tayari Wilaya ya Nyamagana wameshawapeleka baadhi ya watoto shule ambao wanaendelea na masomo na kupata huduma mbalimbali bure.

Aliongeza kuwa kwa sasa changamoto ni mrundikano wa watu katika jiji na kuzishauri halmashauri kuungana kuondoa hali hiyo.

“Tushirikiane kwa pamoja, kwasababu Nyamagana inakuwa na idadi kubwa ya watu kutoka wilaya nyingine kutokana na huduma zilizopo, hivyo lazima tuungane kwa pamoja, vinginevyo kila upande utabeba mzigo wake,” alisema Kotecha.