Wanaohoji kuhusu Muungano kusikilizwa EACJ

Muktasari:

  • Kati ya kesi zinazotarajiwa kuvuta hisia za wengi ni kesi namba 7 ya mwaka 2017 iliyofunguliwa na Rashid Salum Adiy na wenzake 39,999 dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu Muungano itakayosikilizwa na jopo la majaji watatu wakiongozwa na jaji kiongozi Monica Mugenyi.

Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) imeanza kusikiliza kesi zilizofunguliwa na watu binafsi pamoja na mashirika mbalimbali dhidi ya nchi wanachama zilizotarajiwa kusikilizwa kati ya jana hadi Machi 29.

Kati ya kesi zinazotarajiwa kuvuta hisia za wengi ni kesi namba 7 ya mwaka 2017 iliyofunguliwa na Rashid Salum Adiy na wenzake 39,999 dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu Muungano itakayosikilizwa na jopo la majaji watatu wakiongozwa na jaji kiongozi Monica Mugenyi.

Majaji wengine ni Fakihi Jundu na Charles Nyawello ambao watatoa uamuzi wa awali wa mpeleka maombi aliyetaka mahakama hiyo ihamishie kwa muda kikao chake Zanzibar ili kuwawezesha wananchi wengi kuhudhuria.

Taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari na msajili wa mahakama hiyo, Yufnalis Okubo iliitaja pia kesi iliyofunguliwa na Baraza la Habari Tanzania(MCT) itakayosikilizwa Machi 13.

Walalamikaji wengine ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) pamoja na Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) huku mahakama hiyo ikitarajiwa kusikiliza maelezo ya awali juu ya hoja zitakazobishaniwa.

Kesi hiyo ambayo waleta maombi wanadai Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 inaminya uhuru wa kupata na kutoa habari hivyo kukiuka itifaki iliyoanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Pia, Machi 14 itasikiliza kesi iliyofunguliwa na Baraza la Serikali ya Kijiji cha Ololosokwan wilayani Ngorongoro dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Tanzania, ambapo wadai walalamika kukiukwa haki zao kwa kuhamishwa kwa nguvu kwenye kijiji chao chenye hati halali za usajili.

Pia, kesi namba 7 ya mwaka 2016 inatarajiwa kusikilizwa Machi 22 iliyofunguliwa na mhariri mtendaji wa Mseto & Hali Halisi Publishers Limited dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.