Wanaolima mirungi, bangi Same kusakwa

Muktasari:

Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Senyamule alisema jana kuwa kifungo cha miaka 30 kitawahusu wakazi wanaolima mirungi na kuleta madhara kwa afya na kuisababishia Serikali hasara kutokana na kutolipa kodi.

Same. Serikali imetangaza vita dhidi ya wakulima wa bangi na mirungi wilayani hapa Mkoa wa Kilimanjaro.

Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Senyamule alisema jana kuwa kifungo cha miaka 30 kitawahusu wakazi wanaolima mirungi na kuleta madhara kwa afya na kuisababishia Serikali hasara kutokana na kutolipa kodi.

Akikabidhiwa mradi wa Ruvu Muungano uliojumuisha zahanati sita, nyumba mbili za waganga, matangi saba ya kuvuna maji na madarasa 54, ofisi 16 za walimu, vyumba na vyoo vya Chuo cha Ufundi Makanya uliofadhiliwa na shirika la World Vision Tanzania, alisema: “Wafadhili wamefanya kazi kubwa katika kujitolea kujenga chuo hiki cha ufundi.

“Wazazi waleteni vijana kusomea ufundi kuliko kulima mirungi kwani haina faida.”

Alisema sheria imekuwa ikiwaadhibu wanaosafirisha, kuuza na kutumia mirungi huku ikiwasahau wanaolima.

Senyamule alisema wataanza kuwakamata wanaolima na kustawisha mirungi kuanzia Oktoba Mosi mwaka huu.

Mkurugenzi wa World Vision Tanzania, Dk Yosh Kasilima alisema mradi wa Ruvu Muungano umegharimu Sh12.4 bilioni katika ujenzi wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Makanya.