Wanaowapekua wafanyakazi sehemu za siri kuchukuliwa hatua za kisheria

Naibu Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira Anthony Mavunde

Muktasari:

  • Mavunde alikuwa akijibu swali bungeni mjini Dodoma leo kuhusu msimamo wa Serikali dhidi ya matukio ya udhalilishaji wa wafanyakazi  maeneo ya migodini.

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira Anthony Mavunde amesema Serikali itawachukulia hatua waajiri wa migodini wanaowadhalilisha wafanyakazi kwa kuwapekua hadi sehemu za siri, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

Mavunde alikuwa akijibu swali bungeni mjini Dodoma leo kuhusu msimamo wa Serikali dhidi ya matukio ya udhalilishaji wa wafanyakazi  maeneo ya migodini.

 Naibu Waziri Mavunde amesema kumekuwa na matukio ya udhalilishaji kwa wafanyakazi yanayofanywa na waajiri zikiwamo baadhi ya kampuni za Wachina.

Amesema baadhi ya Wachina hao  wamekuwa na tabia ya kusingizia kutojua  Kiswahili kama sababu ya kutofahamu sheria za kazi nchini na kunyanyasa wafanyakazi wao.

Pia, amebainisha kuwa Serikali inatambua kutojua sheria si sababu ya kufanya kosa, hivyo imekuwa ikipokea taarifa kutoka vyanzo mbalimbali kuhusu matukio ya udhalilishaji.

Ameahidi kuwafikisha katika vyombo vya sheria waajiri wanaoendelea kukiuka sheria za kazi nchini.