Wanasayansi watengeneza kinga mpya ya mwili dhidi ya HIV

Muktasari:

  • Shirika linasema chembe chembe hiyo ya kinga imetengenezwa ili kushambulia sehemu tatu muhimu za virusi na kuvifanya vishindwe kuhimili mashambulizi yake

London, Uingereza. Wanasayansi wanaelekea kufanikiwa kutengeneza chembe chembe za kinga ya mwili zinazoweza kushambulia asilimia 99 ya virusi vya vinavyosababisha ukimwi na hivyo kuweza kuzuia maambukizi kuendelea.

Taarifa iliyotolewa na shirika la kimataifa la kukabiliana na ukimwi liitwalo International Aids Society imesema kuwa huu ni "ugunduzi wa kihistoria".

Shirika hilo linasema chembe chembe hiyo ya kinga imetengenezwa ili kushambulia sehemu tatu muhimu za virusi na kuvifanya vishindwe kuhimili mashambulizi yake.

Kazi ya utengenezaji chembe chembe hizo za kinga ya mwili imetokana na ushirikiani baina ya Taasisi ya Marekani ya Afya na kampuni maduka ya dawa ya Sanofi. “Huu ni ugunduzi wa kihistoria,” anasema Dk Gary Nabel, anasema ofisa mkuu wa Sanofi.

Majaribio ya kinga kinga hiyo ya mwili kwa binadamu yataanza kufanyika mwaka 2018 kuangalia kama dawa hiyo inaweza kuzuia au kutibu maambukizi ya HIV

“Miili yetu huhangaika kupigana na virusi vya HIV kwa sababu virusi hivyo vina uwezo mkubwa wa kujibadilisha katika hali nyingine pamoja na mwonekano wake,” inasema taarifa ya shirika hilo.

Kwa mujibu wa shirika hilo, aina kadhaa za virusi vya HIV kwa mgonjwa mmoja zinaweza kufananishwa na zile za mafua wakati wa msimu wa baridi. Kwa hiyo, mfumo wa kinga ya mwili hujikuta katika vita dhidi ya magonjwa kadhaa nyemelezi yanayosababishwa na HIV.

Watafiti wamekuwa wakijaribu kutumia uwezo wa mwili wenyewe wa kupunguza uharibifu wa kinga ya mwili kama njia ya kutibu HIV au kuzuia maambukizi hayo mapema.