Wanaume 50 wakubali yaishe, wapeleka DNA kwa mkemia

Muktasari:

  • Wanawake wamekuwa wakiripoti katika ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ili kupata msaada wa kisheria baada ya kutelekezwa na waume zao.

Ofisa ustawi wa jamii Mkoa wa Dar es Salaam, Flora Masue amesema zaidi ya mashauri ya watu 6,000 yamesikilizwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa, kati ya hayo 50 wahusika wamechukuliwa vipimo vya vinasaba (DNA).

Wanawake wamekuwa wakiripoti katika ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ili kupata msaada wa kisheria baada ya kutelekezwa na waume zao.

Awali, suala hilo lilikuwa ni kwa ajili ya wanawake waliotelekezwa, lakini wanaume nao walitumia fursa hiyo kueleza shida zao huku wanaume waliopelekewa barua za wito nao wakifika.

Hata hivyo, wapo wanaume walioonyesha wasiwasi kuhusu uhalali wa watoto hao hivyo ikaamuliwa kupimwa DNA.

Masue alisema kuanzia Aprili 16 wameanza kuwasikiliza wanaume, waliopewa barua kwenda ofisi ya mkuu wa mkoa huyo.

“Sasa hivi tunasikiliza pande zote mbili, kuna wanaolalamika kutelekezewa watoto na wanaolalamikiwa hadi sasa hivi zaidi ya watu 6,000 wamesikilizwa, kati yao 50 wameshachukuliwa vipimo vya DNA,” alisema.

Mwanasheria wa Serikali, Fabiola Mwingira alisema kuanzia Aprili 13 hadi 15 walikuwa wanawasikiliza wanawake lakini kuanzia Aprili 16 hadi 20 wameanza kusikiliza walalamikiwa.

Miongoni mwa wanaume waliolalamika ni mkazi wa Gongolamboto, Isaya Lameck ambaye amemshtaki mkewe kwa kuambiwa kuwa mtoto wa miaka mitano na mimba ya miezi sita aliyonayo si yake.