Wanawake 1000 wafunga siku tatu, wamuombea Dk Magufuli

Rais Magufuli 

Muktasari:

Mratibu wa kongamano linalohusika na maombi hayo, Deborah Malassy amesema ni kawaida yao kukutana kila mwaka lakini mwaka huu, maombi ni kwa Rais Magufuli kutokana na jinsi anavyoongoza nchi.

Dar es Salaam. Wanawake zaidi ya 1000 kutoka ndani na nje ya nchi wamekutana jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kumuombea Rais John Magufuli huku wakiwa wamefunga siku tatu mfululizo.

Pia wanawake hao wanaoiombea nchi amani na kuiepusha jamii na mmomonyoko unaodaiwa kuwa sababu ya kuongezeka maovu ikiwamo ufisadi na mimba mashuleni.

Mratibu wa kongamano linalohusika na maombi hayo, lililoandaliwa na Tanzania Fellowship of Churches, Deborah Malassy amesema ni kawaida yao kukutana kila mwaka lakini mwaka huu, maombi kwa Rais Magufuli yamekuwa ya kipekee kutokana na namna anavyoongoza.

“Tunamuombea Rais Magufuli ili haya anayoyafanya katika kupambana na rushwa, ufisadi, udhalimu kwa baadhi ya viongozi na mmomonyoko wa maadili afanikiwe na mwisho, amani ya nchi iendelee kutawala. Ajue tupo nyuma yake na tunachofanya ni kutimiza wajibu wetu, tena kwa kufunga kama tunavyofanya,”amesema.

Amesema viongozi wa dini wana jukumu kubwa la kuwakumbusha waumini wao umuhimu wa kuombea taifa lao lirejee katika misingi ya maadili.

Mchungaji huyo alisema ukweli ni kwamba hakuna njia nyingine inayoweza kusababisha amani na utulivu katika taifa isipokuwa kwa maombi, kama walivyoamua kufanya.

Ameongeza kuwa suala la mimba shuleni ambalo limeleta mjadala mkubwa kitaifa linachangiwa kwa kiasi kikubwa na mmomonyoko wa maadili katika jamii.

“Tunalia kwa ajili ya mabinti zetu, ni sisi wanawake tuliojisahau na tunajua Rais Magufuli aliamua kutukumbusha wajibu wetu. Tutatumia muda mrefu kuomba kwa ajili ya hili lakini pia kuchukua hatua za malezi bora kwenye familia,”alisisitiza.

Akifungua kongamano hilo la maombi, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhandisi Stella Manyanya amesema wanawake hao wametimiza wajibu wao wa kumuombea Rais na Serikali yake hasa wakati huu yanapofanyika maamuzi magumu.