Wanawake saba wenye ulemavu waliofanya vitu vya kipekee

Wakonta  Kapunda

Muktasari:

  • Mwananchi imewatathmini wanawake saba wenye ulemavu ambao wamefanya maajabu na kuonyesha kwamba ulemavu wao haukuwa chanzo cha kuzima ndoto zao kimaisha.

Dar es Salaam. Wakati dunia ikiadhimisha siku ya wanawake, wapo wenye ulemavu waliofanya vitu vya kipekee na visivyotarajiwa katika jamii inayowazunguka.

Mwananchi imewatathmini wanawake saba wenye ulemavu ambao wamefanya maajabu na kuonyesha kwamba ulemavu wao haukuwa chanzo cha kuzima ndoto zao kimaisha.

Stella Alex Ikupa

Oktoba mwaka jana, Rais John Magufuli alimteua Stella Ikupa kuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (watu wenye ulemavu).

Ikupa ni mlemavu wa viungo na ni mbunge wa Viti Maalumu anayewakilisha kundi la walemavu.

Amekuwa miongoni mwa wanawake wachache wenye ulemavu kuwahi kushika nafasi hiyo ya juu ya uongozi.

“Ninachoweza kusema kwa wanawake wenzangu kwa siku ya leo ni kujiamini na kutokukata tamaa tu. Katika haya tunayoyafanya tuonyeshe uwezo wetu kwa sababu ni kweli tunaweza bila hata kuwezeshwa,” alisema.

Maria na Consolata Mwakikuti

Maria na Consolata ni pacha walioungana ambao wameishangaza dunia baada ya kufaulu vizuri mitihani yao ya kitaifa kuanzia darasa la saba, sekondari na kidato cha sita. Pacha hawa waliozaliwa Ikonda wilayani Makete Mkoa wa Njombe wamekuwa mfano wa pekee na wameionyesha dunia kwamba, ulemavu si sababu ya kushindwa kutimiza ndoto za kimaisha.

Kwa sasa wanasoma katika Chuo Kikuu cha Katoliki cha Ruaha (Rucu) wakichukua shahada ya ualimu.

Joyce Kantande

Huyu ni mwalimu anayeishi Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam ambaye kwa takribani miaka 19 sasa amekuwa akifundisha wanafunzi akiwa amelala kitandani baada ya kupooza mwili mzima kutokana na ajali ya gari. Alipata ajali hiyo akiwa na umri wa miaka minane.

Pamoja na changamoto hiyo, aliendelea na masomo yake ya sekondari na kumaliza kidato cha nne na baadaye kujiunga na kidato cha tano na sita.

Huku akiwa na maumivu makali ya mgongo alijiunga na Chuo cha Uhasibu alikosomea uboharia.

Juhudi za kupata kazi zilikwama kwa kuwa muda mwingi alikuwa akisaka matibabu na baadaye miguu ikaanza kuwa mizito na kujikuta akiwa mtu wa kulala maisha yake yote.

Kwa kuwa akili yake ilikuwa bado inafanya kazi alitafuta mbinu za kujipatia ajira na hivyo akaanza kuwafundisha watoto wadogo akiwa kitandani chumbani kwake.

Baada ya watoto hao kupata mafanikio ndipo alipofungua darasa na kwa mwaka anapata watoto zaidi ya 50.

Ujasiri wa Mwalimu Joyce unamfanya kuwa miongoni mwa wanawake waliopiga hatua na hivyo kuwazibua wengine akili kwamba, inawezekana.

Wakonta Kapunda

Wakonta aligongwa na gari siku ya mahafali yake ya kumaliza kidato cha nne. Alikuwa akisoma shule ya sekondari ya wasichana ya Korogwe, Tanga.

Ajali hizo ilimjeruhi zaidi uti wa mgongo na kusababisha apooze mwili mzima.

Hata hivyo, Wakonta, mkazi wa Rukwa, anatumia kichwa chake ambacho ndicho kiungo pekee chenye uwezo.

Anatumia ulimi wake kuandika muswada wa filamu ili kujipatia fedha.

Amefanikiwa kuendeleleza ndoto yake ya uandishi wa filamu kwa kutumia ulimi wake, ambao ndio pia anaotumia kujibia simu na kuandika ujumbe mfupi wa simu ya mkononi.

Miriam Stanford

Huyu ni mlemavu wa ngozi, mkazi wa Ngara, Mkoa wa Kagera aliyekatwa mikono miaka 10 iliyopita, kutokana na imani za kishirikina.

Miriam ameonyesha ujasiri kwani licha ya kukosa mikono, anadarizi vitambaa kwa cherehani akitumia miguu yake.

Kadhalika, mwanamke huyo atapanda Mlima Kilimanjaro na wanawake wengine katika kuadhimisha siku ya leo. “Nilikatwa mikono miwili bila ganzi, nimeishi maisha ya hofu lakini sasa ninajiamini na ninaweza kufanya jambo lolote linaloweza kufanywa na binadamu.”

Chekeni Salum

Chekeni Salum ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mkwa, wilayani Masasi ambaye alizaliwa bila mikono yote miwili.

Pamoja na ulemavu huo, binti huyo anamudu kufanya shughuli zake zote za nyumbani na shuleni .

Nidhamu, utii na uwezo wake mkubwa darasani ulimfanya achaguliwe kuwa dada mkuu.

Wanaharakati na viongozi wanasema, dhana finyu kuhusu wanawake wenye ulemavu katika jamii imeanza kuondoka baada ya wachache waliopata nafasi kufanya vizuri.

Mbunge wa Viti Maalumu anayewakilisha kundi la watu wenye ulemavu, Amina Mollel anasema ulemavu si tatizo linaloweza kumfanya mwanamke kushindwa kupiga hatua kimaendeleo ikiwa atapatiwa fursa.

“Ulemavu sio sababu ya kushindwa kila kitu kinawezekana pale fursa inapotokea, tunachoshukuru jamii imebadilika na inaelewa hasa na imeanza kuachana na ile dhana finyu ya unyanyapaa,” alisema.

Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Edda Sanga anasema ili wanawake wenye ulemavu waonyeshe uwezo wao, wanapaswa kushirikishwa.

“Hata kwenye uongozi kuanzia ngazi za vijiji, walemavu wanawake wanapaswa kushirikishwa kwa sababu wakipata nafasi wanaonyesha uwezo wao,” alisema.