Wanawake MCL washerehekea Siku ya Wanawake na mke wa Azory Gwanda

Wafanyakazi wa Mwananchi Communications Limited (MCL) wakipiga picha ya pamoja na mtoto wa Azory,Gladness walipokwenda kumtembelea mke wa Azory, Anna nyumbani kwake Kibiti. Picha na Venance Nestory

Muktasari:

  • Wanawake hao wameiadhimisha siku hiyo pamoja na mke wa Azory Gwanda aliyetoweka.

Kibiti. Wanawake wa Mwananchi Communications Ltd, (MCL) wameungana na wenzao duniani kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani kwa kumtembelea na kumtia moyo mke wa mfanyakazi mwenzao, Azory Gwanda, Anna Panon.

Gwanda, mwandishi wa kujitegemea wa Kampuni ya Mwananchi aliyekuwa anaishi na kuripoti kutoka Kibiti mkoani Pwani alitoweka Novemba 20, mwaka jana na hadi sasa hajulikani alipo.

Akizungumza leo Machi 8 kwa niaba ya wanawake hao, mhariri wa makala za afya wa gazeti la Mwananchi, Lilian Timbuka amesema upendo, umoja na mshikamano ndio uliowafanya kuadhimisha siku hiyo wakiungana na Anna.

Timbuka amesema bado wana imani kwamba Azory yupo mahali salama na ipo siku ataungana na mkewe Anna kuendelea na maisha.

"Upendo ndio uliotukumbusha kuungana na mwanamke mwenzetu Anna leo hii, kikubwa tuendelee kuomba tukitarajia kuna wakati mfanyakazi mwenzetu atarejea,"amesema.

Amemshauri  mke wa  Azory kutokata tamaa katika kuomba na kwamba, nyuma yake wapo wengi wanaomsaidia.

Kwa upande wake, Anna amesema amefarijika kuwaona wanawake wenzake wanaungana naye katika maombi kuhakikisha mumewe anarudi.

Ameishukuru MCL kwa upendo waliouonyesha tangu mumewe alipotoweka.

"Sina cha kuwalipa, zaidi nashukuru mno kwa sababu mmekuwa nami katika kipindi huki kigumu," amesema.

Huku akibubujikwa machozi, Anna amesema anaamini ipo siku mumewe atarejea tena nyumbani

 Wanawake hao wa MCL wamempelekea zawadi mbalimbali mke wa Azory ikiwamo fedha, mahitaji ya watoto na bima za afya kwa ajili ya watoto.