Wanawake wajasiriamali watakiwa kurasimisha biashara

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng’i Issa akimkabidhi mmoja wa wahitimu 510 wa mafunzo ya ujasiriamali, Halima Kinabo Dar es Salaam leo. Wengine ni Afisa Mkuu Mtendaji wa Gatsby Tanzania Trust (TGT) iliyoendesha mafunzo hayo, Olive Luena (kushoto) na Balozi Mdogo wa Uholanzi nchini, Hinke Nauta (kulia).

Muktasari:

Akizungumza jijini hapa jana, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng’i Issa amesema kwa kurasimisha biashara zao, wanawake watajiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kujiendeleza wao, jamii inayowazunguka na taifa zima kwa ujumla.

Dar es Salaam. Wanawake wajasiriamali nchini wametakiwa kuhakikisha wanarasimisha biashara zao ili waweze kupata fursa mbalimbali na kuendelea zaidi.

Akizungumza jijini hapa jana, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng’i Issa amesema kwa kurasimisha biashara zao, wanawake watajiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kujiendeleza wao, jamii inayowazunguka na taifa zima kwa ujumla.

Alikuwa akizungumza katika mahafali ya mafunzo ya ujasiriamali ambapo jumla ya wanawake 510 wa jijini Dar es Salaam walifuzu na kutunukiwa vyeti.

Mafunzo hayo ya miaka mitatu yaliendeshwa na Tanzania Gatsby Trust (TGT) na kufadhiliwa na Comic Relief.

“Ukiweza kurasimisha biashara yako, utafikiwa kwa urahisi na fursa zinazotolewa na Serikali na wadau mbalimbali,” amesema.

Afisa Mkuu Mtendaji wa TGT, Olive Luena alisema wahitimu hao walipata mafunzo kupitia mradi wa “Mkubwa” wa shirika hilo ili kuwaongezea ujuzi na ubunifu wa kibiashara.

Balozi Mdogo wa Uholanzi nchini, Hinke Nauta alisema nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania na pia kusaidia Gatsby Tanzania kukuza wajasiriamali wanawake. 

Kwa taarifa zaidi nunua gazeti lako la Mwananchi au soma mtandaoni kupitia www.epaper.mcl.co.tz