Wanawake wanne wanusurika kuteketezwa kwa moto

Muktasari:

  • Wanawake hao waliopigwa na kujeruhiwa wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora wakiuguza majeraha.

 Wakati kumbukumbu ya wanawake watano waliouawa na wananchi na miili yao kuchomwa moto katika Kijiji cha Undomo wilayani Nzega ikiwa haijafutika, wengine wanne wamenusurika kuteketezwa kwa moto Uyui.

Tukio hilo limetokea katika Kijiji cha Mwamabondo wilayani Uyui ambako wanawake wanne walikamatwa, kupigwa na kuchomwa moto mwilini lakini waliokolewa na polisi kabla hawajateketezwa kwenye lundo la kuni lililokuwa limeandaliwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Wilbroad Mutafungwa amesema leo Jumanne kuwa, tukio hilo lilitokea Septemba 17 katika Kijiji cha Mwamabondo, Kata ya Ioya.

Amesema wanawake hao walikamatwa na wananchi, kupigwa kwa fimbo na kuchomwa baadhi ya sehemu za miili yao.

Mutafungwa amesema wananchi hao walilenga kuwateketeza wanawake hao lakini waliokolea na polisi baada ya taarifa kuwafikia kutoka kwa baadhi ya wakazi wa kijiji hicho.

Amesema wanawake hao ambao walituhumiwa kuwa ni wachawi ni Manugwa Lutema (45), Elizabeth Kashindye (47), Rahel Mikomangwa (53) na Maria Sahani (49), ambao wote wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Kitete kwa matibabu.

Mganga mkuu wa mkoa huo, Dk Gunini Kamba amesema wamejeruhiwa miguuni na kwenye makalio.

Kamanda Mutafungwa amesema ulinzi umeimarishwa katika hospitali hiyo ili wasitokee watu wa kuwadhuru.

Amesema hadi leo Jumatano mchana wameshawakamata watuhumiwa 44 na msako wa kuwatafuta wengine unaendelea.

Miongoni mwa waliokamatwa amesema ni viongozi wa kijiji hicho na kwamba, taarifa za awali zinasema chanzo cha tukio hilo ni mganga wa kienyeji Mafumba Tilawisi (70), kufariki dunia muda mfupi akitoka kwenye shughuli zake za kiganga katika kijiji jirani Septemba 16.

Kamanda Mutafungwa amesema wakati utaratibu wa maziko ukiendelea zilisika tetesi kuwa mke wa marehemu, Manugwa Lutema alihusika kumuua mumewe kwa njia ya kishirikina ndipo wananchi walipompiga wakimtaka awataje wenzake anaoshirikiana nao katika uchawi, hivyo aliwataja wenzake hao watatu.

Amesema wakiwa wamefungwa vitambaa usoni, huku wakiwa watupu kabla hawajawekwa kwenye moto wa lundo la kuni uliokuwa unawaka, ndipo polisi walipofika na kuwaokoa.

Katika tukio la Kijiji cha Undomo, wanawake watano walipigwa na kuchomwa moto na kundi la wanakijiji Julai 25 wakiwatuhumu ni wachawi.