Wanawake watamani kiwanda cha asali

Muktasari:

  • Wanawake hao jamii ya Kimasai zaidi ya 600 kutoka Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara waliunda vikundi 21 vya kufuga nyuki, kurina asali na kuuza.
  • Wanawake hao walisema mwishoni mwa wiki iliyopita walisema shughuli hiyo imekuwa na manufaa kwao, hivyo wanataka kupanua wigo wa biashara.

Simanjiro. Katika kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli za Tanzania ya viwanda, wajasiriamali wanawake wanaozalisha asali, wameiomba Serikali kujenga kiwanda cha kukamua bidhaa hiyo kwa kuwa ina faida kubwa.

Wanawake hao jamii ya Kimasai zaidi ya 600 kutoka Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara waliunda vikundi 21 vya kufuga nyuki, kurina asali na kuuza.

Wanawake hao walisema mwishoni mwa wiki iliyopita walisema shughuli hiyo imekuwa na manufaa kwao, hivyo wanataka kupanua wigo wa biashara.

Mmoja wa wanakikundi hao, Maria Simon alisema kikundi chao kilianza kikiwa na watu 15 na walishindwa kubuni mradi kutokana na kutokuwa na elimu ya ujasiriamali.

“Baada ya semina ya ujasiriamali iliyoendeshwa na Taasisi ya Tanzania People Wildlife (TPW) tulijua mradi wa kuzalisha asali ungetusaidia, hivyo tuliungana kutoka vijiji vitatu tukawa 620, tukaomba ufadhili uliotuwezesha kupata mizinga 10 kwa kila kundi la watu 30.

“Mradi huu umekuwa msaada kwetu kwa kuwa awali tulikuwa tunategemea kilimo na maziwa kutoka kwenye mifugo yetu pekee. Msimu wa ukame tulikosa chakula, lakini sasa tunamiliki mizinga zaidi ya 700, hivyo tunapata fedha za kujikimu kwa mahitaji ya familia kama chakula, ada za watoto shule na mavazi,” alisema Simon.

Aliiomba Serikali kuwawezesha kupata kiwanda cha kukamua asali kwa ajili ya kurahisisha shughuli zao.

Ofisa Elimu ya Mazingira kutoka TPW, Revocatus Magane alisema waliamua kuwanunulia wanawake hao mizinga ili wajipatie kipato cha kujikimu kimaisha.

Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Loibor-Serieti ulipo msitu wa kuendeshea mradi huo, Mathayo Rimba alisema asilimia kubwa ya wanawake wa jamii ya Kimasai wamekuwa nyumbani wakitegemea shughuli za kilimo na ufugaji, hivyo uwapo wa mradi huo umekuwa msaada mkubwa kwao.

“Mradi huu unaoendeshwa na wanawake hawa ni mzuri sana, maana unawasaidia kuwasomesha watoto hasa wa kike ambao bado mwamko wa elimu ni mdogo, hivyo Serikali tunafanya mpango wa kuwawezesha zaidi ikiwamo kuhakikisha mradi huu unakua na kuwa na manufaa kwao,” alisema.