Wanne mbaroni wakidaiwa kumpasua Mghana aliyefia hotelini kumtoa ‘unga’

“Tunajua vita hii ni kubwa lakini tutashinda. Hakuna mtu atakayesalimika, niwatake watuhumiwa waliotajwa wafike polisi kwa sababu hawatasalimika.”

Kamanda Sirro 

Muktasari:

Sirro alisema raia huyo wa Ghana alifariki dunia Machi 14 katika nyumba ya wageni, inayoitwa Red Carpet iliyoko Sinza.

Dar es Salaam. Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, wanawashikilia watuhumiwa wanne kwa kuhusika na biashara ya dawa za kulevya baada ya kudaiwa kukiri kuupasua mwili wa Raia wa Ghana aliyefariki jijini hapa na kutoa dawa hizo.

Kamishna wa kanda hiyo, Simon Sirro alisema watuhumiwa hao walihusika na tukio hilo lililofanyika katika Hospitali ya Mwananyamala baada ya marehemu kufa  akiwa na dawa hizo tumboni.

Sirro alisema raia huyo wa Ghana alifariki dunia Machi 14 katika nyumba ya wageni, inayoitwa Red Carpet iliyoko Sinza.

Alisema mmoja kati ya watuhumiwa hao wanaoshikiliwa kwa mahojiano, alikiri kuuchana mwili wa marehemu na kuchukua kete 32  kwenda kumkabidhi mwenzao.

Sirro alisema baada ya mmoja wa watuhumiwa hao kuchukua kete hizo, alimuuzia mtuhumiwa mwingine ambaye aliwahi kutajwa katika orodha ya waagizaji, watumiaji na wauzaji wa dawa za kulevya mwanzoni mwa mwaka huu.

Alisema uchunguzi unaendelea dhidi ya watuhumiwa hao na utakapokamilika jalada lao litapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kwa ajili ya kufunguliwa mashtaka.

Alieleza kuwa bado mwili wa raia huyo wa Ghana upo chini ya Serikali, huku jitihada za kutafuta ndugu zake zikiendelea kwa sababu ubalozi wa Ghana upo Nairobi nchini Kenya.

Katika hatua nyingine, polisi wanamshikilia mtuhumiwa aliyekamatwa na bastola na risasi mbili kinyume na sheria.

Taarifa za mtuhumiwa huyo zilipatikana kutoka kwa raia wema maeneo ya Kariakoo, baada ya kusemekana anamiliki silaha hiyo.

Sirro alisema baada ya kukamatwa mtuhumiwa alikiri kumiliki silaha hiyo na kuwapeleka alipoifukia Mtaa wa Sharrif Shamba.

Alisema mtuhumiwa aliiba silaha hiyo kutoka kwa mwenye nyumba aliyokuwa akifanya kazi maeneo ya Ukonga Kichangani.