Waonywa kuigeuza Tanzania Dampo la bidhaa zisizo na ubora

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqarro ametoa onyo hilo leo (Jumatatu) alipofungua semina ya wafanyabiashara na mawakala hao, iliyoandaliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Wauzaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi na mawakala wa forodha Kanda ya Kaskazini, wameonywa kuacha kuigeuza Tanzania kuwa dampo la bidhaa zisizo za ubora.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqarro ametoa onyo hilo leo (Jumatatu) alipofungua semina ya wafanyabiashara na mawakala hao, iliyoandaliwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Daqarro amesema wauzaji wa bidhaa kutoka nje na mawakala wa forodha wana wajibu wa kuhakikisha wanafuata utaratibu wa TBS kuhakiki ubora wa bidhaa kabla ya kuletwa nchini.

"Tanzania si dampo la bidhaa zisizo na ubora, hivyo ni wajibu wenu, kuwasiliana na kampuni za uhakiki wa bidhaa zilizoteuliwa na TBS nje ya nchi ili kuhakikisha ubora wa bidhaa kabla ya kuzileta nchini," amesema.

 

Ridhiwani Ramadhani, ambaye ni kaimu mkurugenzi wa udhibiti wa ubora wa bidhaa na mkuu wa ukaguzi wa TBS, amesema ukaguzi wa bidhaa unatakiwa kufanyika nje ya nchi ili kuondoa tatizo la bidhaa zisizo na ubora kuingia nchini.

Amewataka wauzaji wa bidhaa na mawakala wa forodha kuzitumia kampuni za ukaguzi zilizoteuliwa na TBS kuhakikisha hawapati hasara kwa kuingiza nchini bidhaa sisizo na ubora.

Ramadhani amesema TBS itaendelea kuongeza ukaguzi na udhibiti wa bidhaa zisizo na ubora kuingia kupitia mipaka yote nchini.

 

Mfanyabiashara, Rajan Razak ameitaka TBS kuwatangaza kwenye vyombo vya habari mara kwa mara mawakala wa ukaguzi wa bidhaa nje ya nchi na sehemu wanakopatikana ili kuwaondolea tatizo la kutokaguliwa bidhaa zao kabla ya kuingia nchini.