Waonywa kutumia mikopo kununulia khanga

Muktasari:

Ofisa Mikopo wa Benki ya CRDB wilayani hapa, James Martin alisema hayo wakati wa uzinduzi wa Chama cha Akiba na Mikopo (Agape Saccos) Kata ya Ubaruku.

Mbarali. Wakulima na wafanyabishara wa mpunga Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, wameonywa kuacha matumizi yasiyostahili kwa fedha za mikopo, badala yake wawekeze kwenye kilimo.

Ofisa Mikopo wa Benki ya CRDB wilayani hapa, James Martin alisema hayo wakati wa uzinduzi wa Chama cha Akiba na Mikopo (Agape Saccos) Kata ya Ubaruku.

Martine alisema kuna tabia ya baadhi ya wakulima na wafanyabishara kukopa fedha kwa ajili ya ushindani wa michango ya harusi, starehe na kujikuta wakikwama katika urejeshaji.

“Mmefungua milango katika taasisi za fedha, viongozi mnapaswa kuwa na dhamana kwa wanachama wenu wanapohitaji mikopo kwa kutembelea miradi wanayoanzisha,” alisema.

Pia, alisema taasisi za fedha kwa kutambua mchango wa wakulima na wafanyabishara, zimeweka kipaumbele kwa kuviwezesha kupata mikopo vyama vilivyosajiliwa na kutambulika kisheria.

Katibu wa Agape Saccos, Rehema Mwankemwa alisema wana akiba ya zaidi ya Sh35 milioni na kwamba, kuna wanachama 140 kati yao, 90 ni wanawake .

Mkulima Abel Mwambone alisema licha ya kujikita katika kilimo, changamoto ni riba kubwa inayotozwa katika taasisi za fedha.

Mwambone aliiomba Serikali kuwasaidia kuwapa mikopo ya riba nafuu, ikiwamo kuwahimiza maofisa ugani kuwatembelea mashambani.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune, Kaimu Ofisa Tarafa wa wilaya hiyo, Sospeter Silayo aliomba taasisi za fedha kuangalia upya kiwango cha riba kwa wakopaji kupitia vikundi na mtu binafsi kwa sababu wana uhakika wa kurejesha.