Wapanga njama kutumbua uongozi

Muktasari:

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara kijijini hapo juzi, baadhi ya wakazi hao walimtuhumu Mwenyekiti wa kijiji hicho, Hamis Nyamamu kuwa ameshindwa kuweka wazi vyanzo vya mapato na matumizi ya fedha zinazokusanywa na ofisi yake.

Musoma. Wakazi wa Kijiji cha Murangi Halmashauri ya Musoma Vijijini mkoani Mara wamesema wataiomba ofisi ya mkurugenzi kutengua uongozi wa kijiji hicho kwa madai ya kushindwa kuwasomea mapato na matumizi.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara kijijini hapo juzi, baadhi ya wakazi hao walimtuhumu Mwenyekiti wa kijiji hicho, Hamis Nyamamu kuwa ameshindwa kuweka wazi vyanzo vya mapato na matumizi ya fedha zinazokusanywa na ofisi yake.
“Wananchi hatujui ni chanzo kipi kinatoa mapato ni kipi hakitoi na kwa nini, tangu mwaka 2014 hadi mwaka jana hatujawahi kusomewa  mapato na matumizi ya kijiji,”  alidai mkazi wa eneo la Murangi, Mafuru Zaghati.
 Mkazi mwingine, Shukrani Bitta alisema tatizo la kusomewa mapato na matumizi ya kijiji hicho limekuwa sugu kwa zaidi ya miaka 15 bila kupatiwa ufumbuzi.
 Akizungumzia malalamiko ya wanakijiji hao, Nyamamu alisema hawajui utaratibu wa kutoa taarifa za mapato na matumizi ya kijiji ndiyo maana wanalalamika hata wanapoelekezwa hawataki kuelewa.