Wapigakura wataka maendeleo sekta za afya, elimu

Muktasari:

  • Akizungumza juzi wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Chama cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika katika kijiji cha Buligi, mkazi wa kata hiyo, Mbazi Laurence alisema kwamba kukosekana kwa diwani kwa kipindi cha miaka miwili kumesababisha wananchi wakose huduma za maendeleo hasa elimu.

 Wakazi wa Kata ya Senga wilayani hapa Mkoa wa Geita, wamesema diwani atakayeshinda katika uchaguzi aanze na changamoto katika sekta za afya na elimu zinazokwamisha maendeleo.

Akizungumza juzi wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Chama cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika katika kijiji cha Buligi, mkazi wa kata hiyo, Mbazi Laurence alisema kwamba kukosekana kwa diwani kwa kipindi cha miaka miwili kumesababisha wananchi wakose huduma za maendeleo hasa elimu.

Mkazi mwingine, Luciana Nelson alisema kwamba wajawazito hulazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilomita nane kutafuta huduma ya afya, hivyo kuwafanya wengi kutohudhuria kliniki na wengine kujifungulia majumbani kwa kukosa huduma.

Mgombea udiwani wa kata hiyo, Thomas Tumbo (CCM) alisema kuwa nia na lengo la kugombea ni kusaidiana na wananchi katika kuhimiza maendeleo ambayo bado yapo nyuma.

“Jambo la kwanza nitakalofanya ni ujenzi wa shule ya Songambele, watoto wetu wanateseka asubuhi kutembea umbali mrefu. Pia, kumekuwa na msongamano mkubwa darasani, peke yangu sitaweza ndiyo maana nataka tusaidiane kuendeleza elimu katika kata yetu,” alisema Tumbo.

Kata hiyo yenye vijiji vinne ina wakazi zaidi ya 20,000.

Uchaguzi katika kata hiyo unarudiwa baada ya diwani aliyechaguliwa mwaka 2015 Joel Ntunginya kutohudhuria kikao hata kimoja na hivyo kupoteza sifa ya kuwa diwani.

Wakati huo huo mbunge wa Nyamagana jijini Mwanza, Stanslaus Mabula amewashawishi wananchi wa Kata ya Mhandu kumchagua mgombea wa CCM, Sima Constantine.

Akihutubia katika uwanja wa Shule ya Msingi Nyakato wakati wa uzinduzi wa kampeni hizo, Mabula alisema kwamba Rais Magufuli amefanya mambo makubwa katika sekta ya elimu.

“Kata hii ina jumla ya wapiga kura 14,000 na ndani ya wiki moja tumeshawafikia wanachama zaidi ya 11,000 sawa na asilimia 79,” alisema.

Naye mgombea Costantine alisema kwamba amejipanga kuboresha elimu, barabara za mitaani, soko, machinjio pamoja na viwanja vya michezo.