Wolper kuyapeleka maonyesho ya urembo ‘uswahilini’

Muktasari:

  • “Katika kulidhihirisha hili kivitendo hata maonyesho yangu nitakuwa nayafanyia uswahilini kama Mbagala, Manzese, Buguruni, Magomeni.”


Dar es Salaam. Msanii wa Filamu, Jacqueline Wolper, amesema amejipanga kuyapeleka maonyesho ya ubunifu na uanamitindo uswahilini kwa lengo la kuwafikia wasichana wanaokaa maeneo ya huko.

Wolper aliwahi kutamba na filamu ya Family Tears, Tom Boy – Jike Dume, Crazy Desire, Mahaba Niue, ameyasema hayo jana alipokuwa akifanya usaili wa wasichana kumi ambao atawatumia kwenye onyesho lake la mavazi analotarajia kulifanya katika Sikukuu ya Pasaka linalojulikana kama ‘Warembo wa Wolper’.

Akizungumza kabla ya kuanza kwa usaili huo, Wolper amesema amefanya utafiti na kugundua kwamba uswahilini kuna vipaji vingi vya masuala ya urembo lakini hakuna watu ambao wameweza kuwafikia, hivyo yeye ameamua kuwa wa kwanza.

“Katika kulidhihirisha hili kivitendo hata maonyesho yangu nitakuwa nayafanyia uswahilini kama Mbagala, Manzese, Buguruni, Magomeni kwani najua mbali na watu kushiriki kuyaona pia nitakutana na vipaji vipya,”amesema Wolper.

Mbali na kuwasaidia katika kukuza vipaji vyao, Wolper amesema itakuwa njia ya wao kupata fursa za ajira kwa madai kwamba anaamini kati ya atakaowapata kuna watakaokuwa na vipaji nje ya uanamitindo na kutokana na yeye tayari kuwa na jina kubwa itakuwa rahisi kwao kuonwa na watu wengine na kuwachukua kufanya nao kazi.

Pia Wolper, ambaye ni mwanamitindo na mjasiriamali alienda mbali zaidi na kueleza kuwa anataka kuona watoto wa kike wanaacha kutumia urembo wao kwa ajili ya wanaume tu na badala yake kuutumia katika kuwaletea hela.

“Utakuta masikini msichana mzuri anaishia kuolewa au kuwekwa ndani na mwanaume na kubaki kununuliwa kila kitu tena wakati mwingine kwa masimango.

“Lakini naamini kama utamjengea uwezo na kutumia urembo wake vizuri mambo kama haya yatamuepuka na nimepania kuwakomboa kwa kweli katika janga hilo,”amesema msanii huyo.