Warioba ajitosa vita dawa za kulevya

Muktasari:

Akizungumza na Mwananchi jana Jumapili, Jaji Warioba alisema ni wakati mwafaka kwa kila mmoja kusoma sheria kuhusu makosa ya uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya na kuvitaka vyombo vya habari viichambue kuangalia kama inafaa au ina mapungufu.


Dar es Salaam. Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba amelizungumzia sakata la vita ya dawa za kulevya na kuvitaka vyombo vya habari na viongozi watoe elimu na kufanya utafiti wa kina ili kupata suluhisho la tatizo hilo.

Akizungumza na Mwananchi jana Jumapili, Jaji Warioba alisema ni wakati mwafaka kwa kila mmoja kusoma sheria kuhusu makosa ya uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya na kuvitaka vyombo vya habari viichambue kuangalia kama inafaa au ina mapungufu.

“Jamii isi- ‘dili’ na watu walioathirika tu, mnafikiri suala ni kumfunga anayetumia dawa za kulevya au anayefundishwa kutumia dawa za kulevya?” alihoji.

Alisema kama ni utafiti ufanyike kwa wanaosababisha na walioathirika badala ya kujikita na matamko ya viongozi ambayo alisema hayasaidii kulimaliza tatizo hilo.

Jaji Warioba ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alisema ni vyema kama wananchi wakaelekezwa wafanye nini ili kupambana na tatizo hilo badala ya kujikita katika siasa na watu.

Alisema kwa kuwa kuna sheria inayoeleza tatizo ni nini na kuna utaratibu wa namna ya kuitumia, basi wananchi wangefundishwa ili wafahamu kitakachowasibu pindi watakapojihusisha na dawa hizo haramu.

Alisema itafutwe njia ya kushughulikia tatizo la dawa za kulevya badala ya kulumbana na kutoa matamko kwani hayasaidii kumaliza tatizo.

Sakata la dawa za kulevya liliibuliwa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda baada ya kutaja orodha ya watu wanaodaiwa kutumia au kujihusisha na biashara ya dawa hizo. Orodha hiyo iliyotolewa katika vipindi viwili tofauti, Februari 3 na Februari 13 ilijumuisha majina ya wasanii, viongozi wa kisiasa na wafanyabiashara wakubwa.

Miongoni mwa waliotajwa katika orodha hiyo ni Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, mfanyabiashara maarufu na mwenyekiti wa klabu ya soka ya Yanga, Yusuf Manji na Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima pamoja na msanii wa filamu, Wema Sepetu.

Mtindo wa Makonda kutaja majina ya watu uliibua mjadala mzito ambapo baadhi ya wabunge walikosoa kitendo hicho wakidai kuwa ni cha udhalilishaji.

Aidha Jaji Warioba hakupendezwa na jinsi vyombo vya habari nchini vilivyolishikia bango suala la dawa za kulevya na kulihusisha na siasa na kusema kwamba wapo viongozi wengi waliotajwa majina yao kwenye kashfa mbalimbali kipindi cha nyuma na kuharibiwa heshima lakini vyombo vya habari viliona ni mambo ya kawaida.

“Hebu niwaulize, hii ni mara ya kwanza kwa majina kutajwa? Tukianzia ‘list of shame,’ si viongozi waliharibiwa heshima? Mbona hatukuona vyombo vya habari kuwatetea wale walioharibiwa heshima? Kuna viongozi wengi waliharibiwa heshima lakini haikuwa ishu, leo hii kumezidi nini mpaka kutajwa hao waliotuhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya imekuwa ishu?” alihoji.

Alisema wapo viongozi (bila kuwataja) waliowahi kumuita Rais ni kuwa ni uchwara, wengine walimuita dhaifu lakini halikuwa jambo la ajabu.

“Mnasema heshima ya mtu imeharibiwa, je, kumuita rais ni uchwara si ni kumharibia heshima yake?” alihoji.

Alisema linapokuja suala kubwa la kupambana na dawa za kulevya, tatizo lenyewe linakwepwa na watu wanaanza kuibua malumbano.

“Hivi mkimjadili Makonda inawasaidia nini au kama kuna wanaomuunga mkono Makonda na wasiomuunga mkono itawasaidia nini?” alihoji Jaji Warioba.

Pia Jaji huyo alisema kuwa nchi ina matatizo mengi lakini watu wamejikita katika siasa tu.

Alisema hadi bungeni walisema wamedhalilishwa lakini na wao huko nyuma walitoa matamko ya kudhalilisha wenzao na hata kumhusisha rais na dawa za kulevya.

 

Ni vita ya kimataifa

Aliyekuwa Kamishna wa Kitengo cha Dawa za Kulevya nchini, Alfred Nzowa alizungumzia vita hiyo na kusema ni vyema taarifa za watu wanaotuhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya kwa namna yoyote zifanyiwe kazi kwanza kabla ya hatua yoyote.

“Hata Kamishna wa sasa Sianga (Rogers) alisema hili, ni wazo zuri kupata taarifa na kuzichuja na kuangalia kama zina ukweli,” alisema.

Hata hivyo Nzowa alitoa siri ya kufanikiwa katika vita hiyo kuwa ni kuangalia mipaka mikubwa ya kimataifa badala ya nchi au mtu mmoja kufanya peke yako bila kushirikiana na wenzako.

“Kama ni usafirishaji si ndani ya nchi hii moja, inapita nchi nyingi ni ‘Trans-organizational Syndicates.’ Wafanyabiashara hii ni wazuri katika mawasiliano hivyo ni lazima anayefanya vita hii avunje mtandao,” alisema.

Alisema vita vinaanzia huko inakolimwa na hivyo ni vyema kubadilishana uzoefu, mbinu na majina ya wauzaji.

Pi alisema katika kupambana na biashara hii ni lazima wanaopambana wawe na nguvu za ziada, mikakati mipana na nidhamu kwani mapapa wa dawa hizo ni watu hatari.