Wasafiri Udart walalamikia huduma

Muktasari:

  • Walitoa malalamiko yao juzi mbele ya bodi ya wakala wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra).

Wasafiri wanaotumia Mabasi yaendayo Haraka (Udart) wamelalamikia kitendo cha mabasi hayo kushindwa kutoa huduma kama mradi unavyojieleza.

Walitoa malalamiko yao juzi mbele ya bodi ya wakala wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra).

Walisema mabasi hayo yanaposhusha abiria hayapakii na kuondoka bali husababisha msongamano kwenye vituo.

Msafiri Brailey Msangi alisema haridhishwi na huduma ya mwendokasi inayotolewa kwa kuwa muda mwingi wakishashusha abiria hata wakikuta kuna mgonjwa hawamchukui kwa kuwa ni express (haraka).

“Unakata tiketi wanakupa, halafu unasubiri masaa mawili hadi matatu mabasi yakija yakishashusha hayapakii wakati tumeshalipa nauli,” alisema Msangi.

Abiria mwngine, Dk Shija Rajabu alisema changamoto kubwa ya usafiri huo ni abira kujazana kituoni kupita kiasi hasa Kituo cha Gerezani, Kivukoni na Fire kuanzia saa 11 jioni.

“Kuanzia saa 11 jioni usafiri wa kutoka katikati ya mji utaratibu ni mbovu, msongamano ni mkubwa mno ukizingatia kuna magonjwa ya mlipuko,” alisema Dk Shija.

Aliiomba Sumatra isaidie tatizo hilo ili kuwanusuru na magonjwa ya mlipuko yanayoweza kutokea kutokana na msongamano ulioko kwenye vituo hivyo.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Udart, Charles Newe alisema sababu zinazofanya msongamano ni askari wa usalama barabarani kuyasimamisha mabasi hayo kwenye makutano na kuruhusu magari mengine kupita wakati wa asubuhi na jioni.

Mwenyekitui wa bodi ya Sumatra Dk John Ndunguru aliwataka Udart kuboresha huduma zao na kuhakisha kila mtu anakuwa na kadi ili kurahisisha usafiri na kuondoa msongamano.

Mkurugenzi Udhibiti wa Barabara kutoka Sumatra, Johansen Kahatam aliwataka watendaji wote wa Udart kuacha kukaa ofisini badala yake wazunguke kwenye vituo vyote ili kujua changamoto zilizopo.