Wasanii 14 waelekea Nairobi kutangaza kazi zao

Balozi wa Uswisi nchini, Florence Mattli (wa nne kutoka kushoto) akizungumza katika onyesho la sanaa ya uchoraji lililofanyika nyumbani kwake Dar es Salaam.

Muktasari:

Kabla ya safari yao, wasanii hao walioko katika kundi la Tanzania Artist Expo 2016 walipata fursa kuonyesha sanaa zao za uchoraji katika makazi ya balozi wa Uswisi hapa nchini, yaliyopo jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Kundi la wasanii 14 wa sanaa ya uchoraji linaondoka leo kwenda Nairobi, Kenya kwa ajili ya programu ya siku 14 ya kujifunza pamoja na kutangaza kazi zao nje ya mipaka 14.

Kabla ya safari yao, wasanii hao walioko katika kundi la Tanzania Artist Expo 2016 walipata fursa kuonyesha sanaa zao za uchoraji katika makazi ya balozi wa Uswisi hapa nchini, yaliyopo jijini Dar es Salaam.

Amani Abeid, mwakilishi wa wasanii hao ameshukuru jitihada zinazofanywa na Balozi Mattli katika kuinua sanaa hiyo ikiwemo kukubali maonyesho yafanyike katika makazi yake ili kupata fedha za kugharamia sehemu ya mahitaji yao ya safari ya Nairobi.

Aidha, balozi huyo amejitolea kugharamia nusu ya gharama za safari hiyo ili wasanii hao wakaonyeshe kazi zao na kutengeneza mtandao wa kimasoko jijini Nairobi.

Amebainisha kuwa sanaa ya uchoraji hapa nchini inakabiliwa na changamoto lukuki zikiwemo za kitaasisi na kisera. Nyingine ni pamoja na vifaa vya kuchorea kuwa ghali kwani ushuru wa kuviingiza hapa nchini uko juu.

Amewataka wawekezaji kuona kuwa hiyo ni fursa kwani iwapo wataamua kutupia jicho eneo hilo, bei za vifaa zitashuka na kuwa fursa ya kukuza sanaa hiyo kwani vijana wengi watashawishika kujiunga nao.

Kwa mujibu wa ratiba, wasanii hao wataonyesha kazi zao katika maonyesho ya sanaa, kutembelea vituo vya sanaa na studio kwa lengo la kujifunza, kujadili na kuitangaza sanaa ya Tanzania nchini Kenya.

Naye Masoud Kibwana ambaye anaelekea Nairobi amesema kazi zao bado hazijakubalika katika soko la Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine za Afrika Mashariki, ikiwemo Kenya.

“Sanaa hii imeachiwa wageni, wanajitahidi kuisukuma mbele kama ubalozi wa Uswisi unavyofanya. Lakini ni suala la utashi, inatakiwa serikali iingilie kutusaidia,” amesema Kibwana.

Kwa upande mwingine, Balozi Mattli amesema safari ya wasanii hao nchini Kenya itasaidia kukuza soko la kazi zao pamoja na kujenga mtandao na wenzao wa Kenya.

Ameongeza kuwa sanaa ya uchoraji ni taswira halisi ya jamii kwani ina uwezo wa kuonyesha nafasi ya mwanamke katika jamii, changamoto zinazowakabili wasichana kielimu na maisha ya wazee.