Washerehekea miaka 55 kwa kupanda Mlima Kilimanjaro

Muktasari:

Msafara wa wapanda mlima hao ulianza Jumatatu kupitia lango kuu la Marangu, safari ambayo ilizinduliwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe.

Arusha. Wakati Watanzania wakisherehekea miaka 55 ya Uhuru wa Tanganyika, Mkuu wa Majeshi mstaafu, Jenerali George Waitara ameongoza ujumbe wa wanahabari, maofisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na wahifadhi kupanda Mlima Kilimanjaro.

Msafara wa wapanda mlima hao ulianza Jumatatu kupitia lango kuu la Marangu, safari ambayo ilizinduliwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe.

Safari hiyo ambayo inalenga kuhamasisha Watanzania kupanda mlima huo itachukua siku sita na inaratibiwa na Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na kampuni ya utalii ya Zara.

Jenerali Waitara ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Tanapa alihimiza usafi katika mlima huo na kuwataka Watanzania kuupanda.

Meneja Uhusiano wa Tanapa, Pascal Shelutete alisema safari hiyo imekuwa na mafanikio makubwa na kutoa wito Watanzania kujitokeza kutembelea vivutio vya utalii na kupanda mlima huo.