Wasichana watakiwa kujikomboa wenyewe

Muktasari:

  • Rai hiyo imetolewa leo Februari  21 na Katibu wa shirika hilo Grace Shaba wakati wa kutoa taarifa ya maadhimisho ya  siku ya ‘Thinking day’ itakayofanyika Februari 24 mwaka huu.

Shirika lisilo la Kiserikali linaloendeleza wasichana na wanawake nchini (TGGA ) limewataka wasichana hasa wa vyuo vikuu kushiriki katika harakati za kujikomboa kifikra, kiuchumi na kujenga uzalendo.

Rai hiyo imetolewa leo Februari  21 na Katibu wa shirika hilo Grace Shaba wakati wa kutoa taarifa ya maadhimisho ya  siku ya ‘Thinking day’ itakayofanyika Februari 24 mwaka huu.

Amesema  maadhimisho hayo yataenda sambamba na utoaji wa misaada mbalimbali kama sehemu ya kujitolea katika jamii.

“Tutatoa misaada kwa wahitaji mfano kuwasaidia wagonjwa kupata matumizi mbalimbali yakiwemo sabuni, matunda, maji na juisi ili kuwafariji wenzetu wenye uhitaji,”amesema

Mbali na misaada hiyo Grace amesema watashiriki katika huduma za uchangiaji wa damu kwa ajili ya kusaidia wagonjwa, kutoa huduma ya afya kwa kupima shinikizo la damu, sukari, uzito na ushauri.

Huduma nyingine ni utoaji wa huduma ya ushauri kwa wenye matatizo ya kijamii na haki za binadamu, kutoa huduma ya elimu kwa jamii pamoja na kutoa huduma ya lishe.

“Chama chetu kinalenga kupanua uelewa kwa vijana wa kike, uzalendo, majukumu ya nchi yao na kuwa tayari kufanya kazi kwa manufaa ya taifa,”amesema  Grace.

Amesema  pia chama hicho kinadhamiria kujenga ushirikiano wa kitaifa na kimataifa kupitutia kambi za mafunzo, kutembelea na kuwasiliana kwa njia za teknohama.

“Tunapenda kuona vijana wakike wanajikomboa kiuchumi, tunafundisha watoto wa kike kwa sababu wao wanauwezo wa kuwa chachu ya maendaleo katika taifa letu na ndiyo maana tunawafundisha ujairiamali na mafunzo ya uongozi,”ameongeza Grace.

Mkufunzi  Emilliana Stanslausi alisema wametoa mafunzo katika vyuo mbalimbali na wasichana wanahamasika  kwani tayari zaidi ya wasichana 400 wameonyesha nia ya kujiunga.

“Tunachukua wanafunzi vyuoni kwa sababu tunahitaji kuwa na viongozi ambao ni waelewa na wenye upeo kuchanganua mambo kwani tunataka wawe wabunifu, wajitambue na wawe waelewa,” amesema Emilliana.

Amesema wanaamini kuwa msichana ananafasi ya kuelimisha jamii ambapo anaazia ndani ya familia na baadaye jamii kwa ujumla.

“Msichana akijitambua, akijielewa, atakuwa kiini cha maendeleo na hiyo itampa nguvu ya kujiendeleza kimaisha kwani ujasiriamali tunaowafundisha unawapa nafasi ya kujiajiri wenyewe,”amesema.