Wasira ataka mabadiliko Chuo cha Mwalimu Nyerere

Muktasari:

Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Steven Wasira ametaka mabadiliko na kurudishwa kwa mafunzo ya uongozi chuoni hapo kwa wafanyakazi wa Serikali na taasisi nyingine.

Dar es Salaam. Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Steven Wasira ametaka mabadiliko chuoni hapo ikiwemo kurudisha mafunzo ya uongozi kwa wafanyakazi wa Serikali na taasisi.

Wasira ambaye aliteuliwa na Raisi John Magufuli, Septemba 9, 2018 ameyasema hayo leo Septemba 21, 2018 katika kikao chake cha kwanza na bodi ya chuo hicho toka ateuliwe.

Amesema ili kurudisha na kulinda misingi iliyoachwa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere iko haja ya kurudisha mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa Serikali na Taasisi.

“Yako mambo mengi yalioachwa na Baba wa Taifa ikiwemo kusimamia haki na usawa, kutetea wanyonge, kusimamia rasilimali za nchi na kupinga rushwa haya yote ukiwa kiongozi lazima uyasimamie” amesema Wasira.

“Tunataka mtu atakayesoma kwenye chuo hiki akimaliza ajivunie na kuonyesha tofauti kama jina la Mwalimu Nyerere lilivyo kwenye jamii yetu,” amesema.

Amesema wapo wazee wengi waliostaafu ambao walifanya kazi na mwalimu wanao uwezo wa kufundisha maadili ya uongozi kama ilivyokuwa awali.

“Nchi nyingi za Afrika zimepata ukombozi kupitia sisi na asilimia kubwa ya watu walioshiriki ukombozi wa nchi hizo wamepitia chuo hiki ndio maana nasema chuo hiki ni kikubwa kwa Afrika,” ameongeza.

Makamu Mwenyekiti wa chuo, Mashavu Fakin amesema chuo hicho chenye tawi Zanzibar kitahakikisha kinapanua wigo na kutoa mafunzo yatakayoiweka nchi kwenye misingi bora.

“Tutahakikisha tunaboresha taaluma kwenye matawi yetu na kutoa mafunzo yatakayowezesha nchi yetu kuwa kwenye misingi bora inayokubalika,” amesema Fakin.