Wasomi nchini wachambua mikopo ya China kwa Afrika

Muktasari:

  • Hivi karibuni, nchi hiyo ilitangaza kutoa Dola 60 bilioni (Sh137 trilioni) kama mkopo wa kufanikisha miradi ya maendeleo.

Dar es Salaam. Hakuna sehemu inapotajwa suala la miradi ya maendeleo barani Afrika ikakosekana jina la China. Taifa hilo linaloshika nafasi ya pili kwa uchumi duniani, limejitokeza kama mshirika muhimu kwa nchi za Afrika kwa namna linavyomwaga misaada isiyo na masharti magumu.

Hivi karibuni, nchi hiyo ilitangaza kutoa Dola 60 bilioni (Sh137 trilioni) kama mkopo wa kufanikisha miradi ya maendeleo.

Miongoni mwa nchi hizo za Afrika, China imejiweka karibu na nchi za Afrika Mashariki ikitekeleza miradi mikubwa ya ujenzi wa miundombinu na kufungua vitega uchumi.

Imefanikisha ujenzi wa reli ya kisasa(SGR) nchini Kenya iliyogharimu dola3.2 bilioni (zaidi ya Sh7.3 trilioni), huku Rais Uhuru Kenyatta akisaini mikataba mingine ambayo itashuhudia kampuni za China zikijikita kwenye ujenzi wa miradi mikubwa.

Hali kama hiyo imeshuhudiwa pia Tanzania na Uganda ambako China imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya kugharimia miradi ya ujenzi wa miundombinu ya reli, nishati na barabara.

Hata hivyo, uhusiano huo umekuwa ukitiliwa shaka huku wachambuzi wa mambo wakitahadharisha juu ya uwezekano wa nchi hizo kumezwa na China.

Akitoa maoni yake, Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mohammed Bakari alisema nchi za Afrika Mashariki zisitarajie makubwa kutoka China akisisitiza kuwa uhusiano unaoonyeshwa na Taifa hilo hauna tofauti na ule wa nchi za Magharibi.

Alisema nchi za Afrika Mashariki zinapaswa kujiuliza mara mbili kwamba zinataka ushirikiano wa aina gani na zaidi ya yote, zinahitaji kujipanga kunufaika na uhusiano huo vinginevyo zitajikuta zikijuta mbele ya safari.

“Huu ni uhusiano wa kawaida wa nchi maskini na nchi iliyopiga hatua kimaendeleo, hivyo kama zitashindwa kujipanga na kujiuliza nini zinataka kwenye mashirikiano hayo hakuna kipya watakachokipata,” alisema msomi huyo wa Sayansi ya Siasa na Utawala.

“Ngoja nikupe mfano, wakati ule nchi za Kusini Mashariki mwa Asia zilipoanzisha uhusiano na baadhi ya nchi za Asia zilizoendelea kama vile Japan na China, zilikuwa zimejipanga na zilijua nini zinataka na matokeo yake ni kwamba leo nchi hizi zimepiga hatua kubwa kimaendeleo”.

Huku akiendelea kusisitiza haja ya kuwapo umakini wa kimkakati, msomi huyo alisema angalau kwa upande fulani inapokuja suala la uwekezaji nchi za Ulaya zimekuwa na tabia ya kuhamishia pia na ujuzi na teknolojia, lakini kwa China hilo halifanyiki.

“Ni ngumu kuona China ikihamishia teknolojia yake katika nchi za Kiafrika mara nyingi haipendi kuwafundisha wazawa na wanachofanya ni kuja na wataalamu wake na kisha kuondoka nao”.

Kuhusu kama China inaweza kutoa mchango mkubwa wa maendeleo ya viwanda katika nchi za Afrika Mashariki, msomi huyo alisema hilo ni gumu kudhihirika kwa vile miradi mikubwa inashikiliwa na raia wa kigeni.

“Angalia mathalani, kama sekta ya hoteli ambayo haihitaji teknolojia, wamiliki wake ni raia wa kigeni. Labda katika eneo letu Kenya kidogo wanaweza kufaidika kwa vile kuna raia wengi hata kama watakuwa na asili ya Asia au Kizungu, lakini wanajitambulisha kama ni Wakenya na wamekuwa kwenye viwanda vingi.”

Katika mkutano wa hivi karibuni kati ya viongozi Afrika na China uliofanyika mjini Beijing, kwa mara ya kwanza katika historia yake, China ilisema itatenga dola5 milioni ili kukuza uingizaji bidhaa za Afrika nchini China.

Hata hivyo, Profesa Kitojo Wetengere wa Chuo cha Diplomasia (CFR), Dar es Salaam alisema jambo kubwa inalolifanya China ni kusaka masoko kwa ajili ya bidhaa zake kupenya katika soko la Afrika na si vinginevyo.

Alisema ingawa diplomasia ya uchumi inasema kila nchi inamhitaji mwenzake pasipo kujali ukubwa wa kiuchumi, lakini China haiwezi kutazamwa kama rafiki aliye na nia njema kwa Afrika.

“Nchi zetu zisidanganyike kuwa China inataka kutusaidia... inataka rasilimali kulisha viwanda vyake na wakati huohuo, inatafuta soko huku kwetu maana ukiangalia hakuna ujuzi wowote inatuletea mbali ya kuja na watu wake wanaoendesha miradi mikubwa.”

Alisema nchi za Afrika zisifurahie kuona zikikopeshwa kitita kikubwa cha fedha, bali zitafakari namna vitakavyoweza kulipa. “Nadhani sisi tunahitaji wataalamu watuletee teknolojia, hizi fedha walizotukopesha tunaweza kuzizalisha hapa kwetu,” alisema.