Wasomi wachambua kujiuzulu viongozi Afrika

Muktasari:

  • Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, wachambuzi hao wamesema viongozi wa nchi mbalimbali, hasa za Kiafrika wanatakiwa kutambua kuwa wananchi wamechoshwa na vitendo vya unyanyasaji na kujilimbikizia mali wakati wao wakikabiliwa na umasikini uliokithiri.

Mabadiliko ya lazima ya viongozi katika baadhi ya nchi za Afrika huenda yakawasomba wengi zaidi sawa na ilivyokuwa wakati wa vuguvugu la kisiasa lililozitikisa nchi za Kiarabu mwaka 2011, wachambuzi wa siasa wameeleza.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, wachambuzi hao wamesema viongozi wa nchi mbalimbali, hasa za Kiafrika wanatakiwa kutambua kuwa wananchi wamechoshwa na vitendo vya unyanyasaji na kujilimbikizia mali wakati wao wakikabiliwa na umasikini uliokithiri.

Wakati Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa (UOI), Dk Jimson Sanga akisema hali hiyo inatoa ujumbe kwa viongozi wa Afrika kuwa wananchi wamechoshwa na vitendo vya unyanyasaji na kulimbikiza mali, Mwenzake Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Ruaha, Iringa, Profesa Gaundence Mpangala anasema matukio hayo yanaashiria pia mageuzi katika bara la Afrika.

Hoja za wasomi hao zinahitimishwa na Profesa Benson Bana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kuwa vuguvugu linaloendelea Afrika ni dalili kwamba demokrasia imezidi kuimarika.

Wataalamu hao wa masuala ya siasa walikuwa wanajadili hatua za ghafla za marais wa Zimbabwe Robert Mugabe, Jacob Zuma wa Afrika Kusini na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Haile Mariam Desalegn kulazimika kujiuzulu kutokana na sababu mbalimbali.

Kauli za wachambuzi

Akifafanua hoja yake, Dk Sanga alisema, “Asilimia kubwa ya viongozi waliong’olewa ama wanang’ang’ania madaraka, mfano mzuri kwa Mugabe au wametumia vibaya rasilimali za nchi kama Zuma wa Afrika Kusini,” alisema alipozungumza na Mwananchi.

Alisema kilichotokea Zimbabwe ni mgogoro wa kiutawala na kwamba, Mugabe ndiye aliyesababisha nchi hiyo kutengwa baada ya kuwafukuza Wazungu, jambo lililosababisha uchumi kudorora na wananchi kujikuta hawana ajira, fedha haina thamani na umaskini ukakithiri huku yeye akijilimbikizia mali.

“Zuma aliingia madarakani kwa mizengwe, nilishuhudia hili wakati huo mimi nikiwa mwanafunzi pale Afrika Kusini, katika utawala wake alitumia vibaya madaraka na kujihusisha na vitendo vya rushwa jambo lililowaudhi wananchi,” alisema.

Sanga anasisitiza kuwa viongozi wanapaswa kujifunza kuwa wawapo madarakani hawana budi kutekeleza demokrasia ya kweli, kutoa haki sawa na kutojihusisha na vitendo vya rushwa, lakini pamoja na vuguvugu lote hilo bado kuna viongozi Afrika wametia pamba masikioni na kujifanya hawaoni kinachoendelea.

Dk Sanga anaungwa mkono na Profesa Mpangala anayesisitiza kuwa matukio hayo yanaashiria mageuzi katika bara la Afrika.

Profesa Mpangala anasema wananchi wanataka demokrasia halisi kwa kuwa wamechoshwa kuminywa, kunyanyaswa na kuwatumikia watawala pekee.

“Nchi nyingi ikiwamo Tanzania ziliamua kuachana na mfumo wa vyama vingi ambao tuliamini hauna demokrasia ya kweli tukaingia wa chama kimoja ili kujenga demokrasia, matokeo tukajikuta tunaingia katika udikteta, ikabidi turudi tena katika vyama vingi.”

“Sasa ni zaidi ya miaka 20 lakini hakuna jipya, wananchi wanaona wamekosea kwa kuwa demokrasia inaminywa, ndiyo wameanza kudai demokrasia halisi ndani ya vyama vingi,” alisema.

“Ukiangalia Zimbambwe, Mugabe alitolewa kwa sababu ya kung’ang’ania madaraka huku akitumia chama chake na vyombo vya dola, ila ikafika wakati navyo vilichoka kumbeba kwa kuwa wananchi walikuwa na nguvu,” alisema.

“Ukija kwa Zuma tatizo kubwa ni ufisadi na kujilimbikizia mali, huku wananchi wake wakiwa katika dimbwi la umaskini, na Ethiopia udikteta umesababisha wananchi kuchoshwa, huku ajira ikiwa tatizo kubwa.

Aliwataka viongozi ambao nchi zao hazijaingiwa na vuguvugu hilo kujifunza na kuweka mfumo, katiba na misingi itakayoweza kutoa haki na usawa kwa wote.

“Hata kama unaona kuna watu wanakupenda lazima uzingatie ukomo wa Katiba mliojiwekea, wananchi wanafika mahali wanachoka,” alisema.

Profesa Bana naye hakuwa mbali na wenzake, akisema vuguvugu la Afrika ni dalili kwamba demokrasia imezidi kuimarika na huu ni mwanzo kwa kuwa kuna uwezekano wa vuguvugu hilo kuambukiza nchi nyingine.

“Hiki ni kielelezo kwamba wananchi wamechoshwa na katiba walizonazo kwa kuwa hazina manufaa kwao na sasa wameamua kupaza sauti ambayo imeanza kusikika. Tunapaswa kuzisuka upya katiba zetu, hali imebadilika, tusipuuze.”

Alisema viongozi wanapaswa kujifunza kwa yanayotokea sasa kuwa, uongozi ni utumishi wa umma na wasitangulize mbele masilahi yao.

“Mifano ipo mingi, unakuta kiongozi hata hapahapa Tanzania, tunashuhudia viongozi wetu wakijilimbikiza mali, majumba ya mabilioni, magari ya kifahari lakini nyendo zao pia si nzuri, hili si jambo jema hata kidogo,” alisema.

Alisema, “Viongozi wanaminya demokrasia, tunashuhudia matendo ya unyanyasaji dhidi ya upinzani, uchaguzi usiokuwa wa haki, ipo siku wananchi wanachoka hii ni wake-up call, ipo siku hali itabadilika.”

Yanayoendelea Afrika

Mapema wiki jana Zuma alijiuzulu kutokana na shinikizo la chama chake cha ANC baada ya kukabiliwa na tuhuma za ufisadi.

Baada ya Zuma kujiuzulu, nafasi yake ilichukuliwa na makamu wake, Cyril Ramaphosa.

Robert Mugabe

Aliyekuwa Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe mwishoni mwa mwaka jana alilazimika kujiuzulu kwa shinikizo la jeshi la nchi hiyo.

Mugabe (93) alitangaza kujiuzulu wadhifa huo muda mfupi baada ya Bunge kuanza utaratibu wa kumwondoa madarakani baada ya utawala wa miaka 37.

Jeshi liliingilia kati mgogoro wa kisiasa nchini humo baada ya Mugabe kumfukuza kazi makamu wake, Emmerson Mnangagwa aliyekuwa anatazamiwa kumrithi katika uongozi wa chama na urais ili kufungua njia kwa mkewe, Grace Mugabe kuchukua nafasi hiyo.

Haile Mariam Desalegn

Kabla vumbi halijatulia, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Haile Mariam Desalegn alijiuzulu wiki iliyopita.

Anasema amechukua uamuzi huo kuiruhusu nchi ifanye mabadiliko yanayohitajiwa na wananchi yatakayoleta amani ya kudumu na demokrasia ya kweli.