Monday, December 19, 2016

Wasomi wafafanua chanzo uhaba wa ajira

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu , Kazi,

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu , Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde. 

By Prosper Kaijage, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wachumi waliotoa maoni yao kuhusiana na tatizo la ukosefu wa ajira nchini wamesema linasababishwa na hali ya uchumi na vijana kutofahamu matakwa ya waajiri.

Maoni hayo yametolewa baada ya Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu , Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde kusema asilimia 67.1 ya vijana wa kati ya miaka 15 hadi 35 hawana ajira.

Mavunde alinukuu Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika mwaka 2012.

Akitoa maoni yake kuhusu changamoto hiyo, Profesa Haji Semboja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema hali ya uchumi kwa sasa haiwatengenezi vijana kuwa tayari kumudu soko la ajira.

Profesa Semboja ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya uchumi, alitoa mfano wa baadhi ya vijana wanaofanya kazi za vibarua.

Kushindwa kuendelea na kazi kwa sababu ya kulipwa ujira mdogo.

Alisema viwanda vingi vipo kwa ajili ya kutengeneza fedha na siyo kutoa ajira zenye tija kwa kundi kubwa.

Pia, alisema ajira nyingi zinazotolewa siyo rasmi.

Profesa Sembojo alisema kama hali ya uchumi ingekuwa nzuri, vijana wengi wangepata ajira rasmi ambazo zingewawezesha kupata malipo mazuri ambayo yangewahamasisha kubaki kazini.

Mtaalamu wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi alisema Serikali inapaswa kutambua sababu ya ukosefu wa ajira ili kutatua changamoto hiyo.

Alisema kwa sasa ni vyema vijana wakajengewa uwezo kulingana na matakwa ya waajiri.

“Suala la ajira ni gumu linapaswa kuchukulia kwa umakini mkubwa,” alisema.

-->