Wasomi wataka wataalamu wa nje waje kusimamia mikataba

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana

Muktasari:

  • Wamesema Tanzania imekuwa ikiingia mikataba mibaya kwa sababu haina wataalamu wa kujadiliana na kujenga hoja za kulinda rasilimali za nchi kwa manufaa ya wananchi wote.

Dar es Salaam. Siku moja baada ya kamati mbili za Bunge kuwasilisha ripoti zake kwa Spika Job Ndugai, wasomi na wanasiasa nchini wameitaka Serikali kuajiri washauri waelekezi kutoka nje kabla ya kutia saini mikataba inayohusu rasilimali za Taifa.

Wamesema Tanzania imekuwa ikiingia mikataba mibaya kwa sababu haina wataalamu wa kujadiliana na kujenga hoja za kulinda rasilimali za nchi kwa manufaa ya wananchi wote.

Juzi, Spika Ndugai alikabidhiwa ripoti na kamati mbili alizoziunda kuchunguza gesi asilia na uvuvi katika bahari kuu. Ripoti hizo ziliibua maovu yanayofanyika hasa kwenye mikataba inayoingiwa na Serikali na kulisababishia Taifa hasara.

Akizungumzia ripoti hizo jana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema dosari kubwa ambayo inalikabili Taifa ni kutokuwa na watu wenye uwezo wa kuzungumza kwa hoja za kutetea masilahi ya Watanzania.

Alishauri Serikali iajiri watu wenye uwezo huo kutoka nje kwa sababu wana uzoefu na wamekuwa kwenye sekta hiyo kwa muda mrefu. Alisema jambo hilo litasaidia kuhifadhi rasilimali za Watanzania.

Dk Bana alisema hakuna haja ya kuharakisha kusaini mikataba wakati haina masilahi kwa nchi. Alitaka mikataba iwe wazi na ikibidi wananchi washirikishwe kwa namna yoyote ili kufikia uamuzi sahihi.

Mwanazuoni huyo alisema, “Kwenye masuala ya mikataba wenzetu wako sensitive sana, wanawashirikisha wananchi ikiwezekana hata kwa referendum (kura ya maoni) ili mradi wahakikishe mkataba unakuwa na manufaa,” alisema Dk Bana.

Akiwa na mtazamo huo, aliyekuwa katibu mkuu wa chama cha NCCR Mageuzi, Samuel Ruhuza alisema mikataba mibovu inasababishwa na kukosekana kwa wataalamu wa kushauri na Serikali kuwaamini wanasheria licha ya kwamba hawana uwezo kwenye masuala ya rasilimali hasa ya gesi asilia.

“Inapofikia hatua ya negotiation (majadiliano), sisi hatuna uwezo, basi tuajiri watu. Wapo waliosoma kwa ajili hiyo. Siyo kila mwanasheria ana uwezo wa ku-negotiate. Kwenye Brexit, Uingereza imeajiri mshauri mwelekezi kutoka Australia ili awasaidie kujiondoa Umoja wa Ulaya,” alisema mwanasiasa huyo.

Kuhusu uvuvi wa bahari kuu, Ruhuza alisema Watanzania wana uwezo wa kuvua katika bahari kuu lakini hawajawezeshwa na Serikali kupata meli kubwa. Alishauri wavuvi wapewe mikopo mikubwa, wapate meli ya kisasa ili wawe na uwezo wa kuvua bahari kuu.

“Huwa tunaambiwa kwamba kuna meli nyingi bahari kuu lakini hazilipi chochote. Hatuna vyombo thabiti vya kufuatilia. Hatuna mipango ya kuwainua wavuvi wetu,” alisema Ruhuza na kuilaumu Serikali kuwa ndiyo iliyolifikisha Taifa hapa lilipo.

Ruhuza alikosoa utaratibu wa Spika Ndugai kuikabidhi Serikali ripoti za kamati alizoziunda akisema zilitakiwa kujadiliwa bungeni na Bunge kutoka na mapendekezo ambayo Serikali ingeyafanyia kazi.

Ruhuza alisema utaratibu wa Spika unaonyesha kama anafanya kazi na Serikali kwa sababu wabunge hawajapata nafasi ya kuzisoma ripoti hizo, kuzijadili na kutoa mapendekezo kwa ajili ya utekelezaji.

“Hii ni ripoti ya wabunge, wanatakiwa waijadili na kutoa mapendekezo. Huenda kuna mambo mengi yameachwa, wangejadili wabunge wangepata nafasi ya kuongeza mengine. Wazo la Spika ni jema lakini tatizo ni finishing (umaliziaji),” alisema mwanasiasa huyo.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi alishauri Serikali kutekeleza mapendekezo yanayotolewa na kamati za Bunge na zile za kitaalamu kwa sababu zinakuwa zimeona mambo mengi na kupendekeza suluhisho.

Alisema, “Hayo yanayopendekezwa na wataalamu ni muhimu na ni vyema yakatekelezwa kitaalamu ili kuepusha kujirudia kwa makosa yaliyofanyika awali au kwenye sekta nyingine tofauti.”

Profesa Haji Semboja wa UDSM, pia alizungumzia kutumia wataalamu wa nje ya nchi akisema siyo jambo baya kwa sababu hao wanaelewa kila kitu kwenye sekta ya gesi, kwa maana ya teknolojia, soko, uwekezaji, uzalishaji na sheria nzuri.

Profesa Semboja alimpongeza Rais kwa kuhakikisha kwamba Tanzania inakuwa na sheria nzuri lakini akamtaka ateue taasisi zenye watu sahihi ambao wamejitoa kulinda na kutetea rasilimali za Taifa.

“Jambo muhimu ni kuweka wazi katika sheria na mikataba yetu kwamba wananchi ndiyo wamiliki na wanufaikaji wa rasilimali zote zilizopo katika nchi yao,” alisema Profesa Semboja ambaye pia ni mtaalamu wa uchumi.