Wastaafu walilia mafao, uongozi wa TRL wawaruka

Muktasari:

Wastaafu hao ambao wameungana kudai stahiki zao walistaafu tangu mwaka 2012 hadi Juni, miaka yote wamekuwa wakidai stahiki hizo bila mafanikio.

Morogoro. Baadhi ya wastaafu wa Shirika la Reli Tanzania (TRL) wamemuomba Rais John Magufuli kuingilia kati na kuwasaidia ili waweze kulipwa mafao yao na fedha za kusafirishia mizigo ambazo wanadai kwa zaidi ya miaka mitano sasa.

Wastaafu hao ambao wameungana kudai stahiki zao walistaafu tangu mwaka 2012 hadi Juni, miaka yote wamekuwa wakidai stahiki hizo bila mafanikio.

Wakizungumza na gazeti hili jana, wastaafu hao walisema madai yao makubwa ni fedha za kusafirisha mizigo na familia ili kurejea vijijini kwao.

Katibu wa wastaafu hao, Selungwi Ubwe alisema wapo zaidi ya 100 katika mikoa mbalimbali nchini ambao wameshindwa kurejea makwao kwa kukosa fedha.“Madai yetu ni nauli za kusafirisha familia na mizigo, mafao ya kustaafu, kuna utaratibu wa wastaafu kulipwa tuzo za ustaafu ambazo ni mabati na mifuko 50 ya saruji na fedha taslim kulingana na kiwango chako cha mshahara na muda uliotumikia shirika,” alisema Ubwe.

Naye mstaafu mwingine, Ally Makubi alisema shirika halina budi kuwalipa stahili zao zote kwani walikuwa waadilifu kipindi chote cha utumishi.

“Mfanyakazi anapostaafu hana tegemeo lolote zaidi ya mafao na tuzo ili aweze kuendeleza maisha mengine, hivyo ni vyema Serikali ikaona umuhimu wa kutulipa tena kwa haraka,” alisema Makubi.

Akizungumzia suala hilo, katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (Trawu), Christopher Kaziyo alisema kwa sasa wameomba kuwasiliana na mkurugenzi wa Mfuko wa Pensheni (PPF) ili kujua tatizo, kwa kuwa ndio unaopaswa kuwalipa pensheni wastaafu hao. “Suala la mafao sheria zipo wazi kama mwajiriwa akithibitisha makato ya fedha hizo kwenye mshahara wake anastahili kulipwa bila kusumbuliwa,” alisema Kaziyo.

Naye mkurugenzi wa TRL, Masanja Kadogosa alisema hakuna mstaafu yeyote anayedai fedha za kusafirisha mizigo na familia kwani hulipwa baada tu mtumishi anapostaafu.

“Hakuna mtumishi anayetudai fedha za kusafirisha mizigo, kwani fedha hizi hulipwa mwanzo kabisa na kuhusu mafao mifuko ya hifadhi ndio inayopaswa kuwalipa,” alisema Masanja.

Mkurugenzi huyo alisema fedha ambazo wastaafu hao hawajalipwa ni za tuzo ambazo zina utata kidogo, hivyo wapo katika majadiliano ili zilipwe.

Uboreshaji TRL

Kampuni hiyo ilianza uendeshaji wa shughuli zake Oktoba 2007 chini ya umiliki wa mwekezaji kampuni ya Rites ya India ambayo ilikuwa inamiliki hisa 51 na Serikali ya Tanzania hisa 40. Hatua hiyo ilifuatia kuvunjwa kwa Shirika la Reli Tanzania (TRC) na kukaribisha wawekezaji ambao baadaye walishindwa na kuanzia Julai 22, 2011 hisa zote za kampuni hiyo zinamilikiwa na Serikali.

Kwa sasa Serikali imedhamiria kuboresha wa miundombinu ya treni na kupitia kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (Rahco), tayari imeingia mkataba na kampuni ya Yapi Merkezi ya Uturuki kujenga kipande cha pili cha reli ya kisasa ya Standard gauge (SGR) kutoka Morogoro hadi Makutopora yenye umbali kilomita 336 za njia kuu na kilomita 86 za njia za kupishana treni zitakazogharimu Sh4.3 trilioni.