Wataalamu wa afya waudadavua ugonjwa wa Mbowe

Muktasari:

  • Watu wengi hupata fatigue kutokana na shughuli zao za kila siku na bila kujua hali hiyo huwasababishia athari mbalimbali kimwili na kiakili.

Siku moja baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuruhusiwa kutoka hospitali ambako ilielezwa kwamba alikuwa akisumbuliwa na uchovu kupita kiasi (fatigue), madaktari na wanasaikolojia wameeleza athari zinazojitokeza mtu anapokuwa na hali hiyo.

Watu wengi hupata fatigue kutokana na shughuli zao za kila siku na bila kujua hali hiyo huwasababishia athari mbalimbali kimwili na kiakili.

Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alilazwa kwa siku moja katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC Moshi, Machi 4 baada ya kuugua ghafla alipokuwa akipata chakula na viongozi wenzake katika Hoteli ya Keys mjini Moshi.

Ofisa Habari wa KCMC, Gabriel Chisseo alisema taarifa za kitabibu zinaonyesha kuwa kilichomsumbua Mbowe ni uchovu. “Tulimpokea akiwa na maumivu makali ya kichwa.”

Aliwekewa oksijeni ili kuidhibiti hali yake kabla ya kupata nafuu na kuruhusiwa.

Kuugua huko kwa Mbowe, kuliibua hoja kadhaa kutoka kwa wataalamu wa afya kuhusu namna uchovu unavyoweza kuleta athari za kiafya pamoja na chanzo cha hali hiyo.

Mtaalamu wa saikolojia, Dk Prinus Saidia alisema mtu anayepatwa na hali hiyo yupo katika hatari ya kuamsha maradhi aliyokuwa nayo hata kama yalitulia.

Alisema kama ana shinikizo la damu au sukari inaweza kupanda kwa sababu mwili unakuwa dhaifu.

“Ndiyo maana watu wanaoumwa maradhi kama hayo na mengine hutakiwa kupata muda mwingi wa kupumzika kuepuka mambo kama hayo,” alisema.

Alisema aghalabu fatigue husababishwa na kufanya kazi kupita kiasi na kuchoka. Alisema wanaofanya kazi zenye hekaheka nyingi na wanaofanya mambo mengi kwa wakati mmoja, hukumbwa na uchovu kupita kiasi.

Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani ya mwili, Meshack Shimwela alisema baadhi ya watu hupatwa na hali hiyo wakiwa na sonona (depression).

“Sonona pia huuchosha mwili, wakati mwingine ikizidi mwili huchoka kupitiliza. Ili utoe tiba sahihi, wenye tatizo hilo lazima wakutane na daktari afanye vipimo na akibaini hawana tatizo zaidi ya fatigue atatoa ushauri au tiba kulingana na hali ya mgonjwa,” alisema Dk Shimwela.

Alisema kama ni uchovu kupita kiasi basi tiba sahihi ni kupumzika na kunywa maji mengi na kusisitiza kuwa kupumzika siyo hiyari bali ni lazima, kwani mwili unahitaji muda wa kupumzika.

Mtaalamu wa saikolojia, Dk Isaac Lema alisema ugonjwa huo ni dalili ya msongo wa mawazo. Alisema dalili zipo tofauti, ila walio wengi huwa ni msongo wa mawazo akidokeza kuwa dalili za uchovu kupita kiasi ni maumivu ya mgongo na kichwa.

“Maumivu makali ya kichwa na mgongo... makali kiasi cha anayeumwa kushindwa kuvumilia, ingawa siyo maumivu yote ya aina hii huwa ni fatigue, inabidi ithibitishwe na daktari,” alisema Dk Lema.

Alisema hali hiyo hutokana na mwili kufanya kazi kupita uwezo wake au muda mrefu bila kupumzika, hivyo akili kufanya kazi kuliko uwezo wa kawaida na kuumiza hisia pia.

“Kwa kawaida kuna baadhi ya vitu mwilini hufanya kazi pamoja. Kazi karibu zote huhusisha akili na hisia kwa sababu bila akili huwezi kujua unafanya nini na bila hisia huwezi kufanya maamuzi ya unachokifanya kwa wakati huo. Hivyo ukichoka kwa kufanya kazi muda mrefu na akili na hisia pia zinachoka kwa sababu vinashirikiana,” alisema Dk Lema.

Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema alisema hali ya Mbowe imeimarika na anaendelea vizuri. “Tunamshukuru Mungu mwenyekiti anaendelea vizuri na kwa sasa yupo mapumzikoni,” alisema Lema.

Fatigue ni hali ya uchovu ambayo mtu huhitaji mapumziko kutokana mwili kukosa nguvu. Fatigue husababsiwa na kufanya kazi kwa muda mrefu bila kupumzika, kutopata muda wa kulala, hofu, kutofanya mazoezi au uchovu.