Wataalamu wa takwimu Afrika wajipanga nchini

Dar es Salaam.Wataalam wa takwimu kutoka mataifa 35 ya Afrika wamekutana jijini Dar es Salaam katika semina maalum kujadili njia sahihi za kukusanya takwimu za ajira barani Afrika.

Semina hiyo iliyoandaliwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) ni sehemu ya maandalizi ya mkutano mkuu wa dunia wa takwimu za ajira utakaofanyika Oktoba mwaka huu mjini Geneva.

Akifungua semina hiyo Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Antony Mavunde amesema takwimu hizo ni muhimu kwa Serikali ili kuiwezesha kuweka mipango yake kwa uhakika.

Alisema Serikali hutegemea kwa kiasi kikubwa takwimu hizo kuandaa sera ya kazi na ajira na kukabiliana na changamoto ya uhaba wa ajira hasa kwa vijana.

“Kwa nchi ambayo inataka kufikia uchumi wa kati takwimu hizi ni muhimu mno. Lazima ujue kuna ajira kiasi gani na uhaba uko vipi ili kujipanga namna ya kukabiliana na changamoto hiyo,”amesema