Sunday, November 19, 2017

Watafiti watatu wasimamishwa kazi sakata la salfa

 

By Elias Msuya, Mwananchi emsuya@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Watafiti watatu wa Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu (TPRI) mkoani Arusha wamesimamishwa kazi kutokana na sakata la ubora wa kiuatilifu aina ya falcon sulphur dust iliyoingizwa nchini kwa ajili ya korosho.

Wakati watafiti hao wakiwa nyumbani, Serikali imeombwa kuunda kamati huru ya wataalamu wa maabara kuchunguza salfa hiyo ili kubaini aliyetoa matokeo yenye walakini kati ya Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na TPRI.

Watafiti hao, Efania Kimaro, aliyekuwa mkurugenzi wa TPRI na Tano Haghai na mwingine mmoja, walifanya uchunguzi wa salfa hiyo na kubaini kuwa haijakidhi viwango.

Walipotafutwa na gazeti hili kuzungumzia suala hilo, Kimaro alisema hawezi kulizungumzia kwa kuwa yupo nje ya ofisi, hivyo waulizwe waliopo, kauli iliyotolewa pia na Haghai. Mtafiti mwingine aliyesimamishwa, hakupatikana kuzungumzia suala hilo.

Wiki iliyopita, Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba aliliambia gazeti hili, alielekeza atafutwe katibu mkuu wa wizara, Mhandisi Mathew Mtigumwe ambaye alisisitiza uamuzi wa kuwasimamisha kazi watafiti hao.

“Hakuna kiuatilifu kinachokwenda kwa mkulima bila kupitia kwenye vipimo. Kwa utaratibu ni lazima kwanza viuatilifu vipelekwe TPRI au kwa Mkemia Mkuu wa Serikali. Hiyo salfa ilichekiwa na ikapitishwa,” alisema Mtigumwe.

“TPRI walipima kwa kutumia ‘specifications’ zao bila kujali mkataba kati ya Bodi ya Korosho na kampuni ya ETG. Ndiyo maana tulimsimamisha kazi mtendaji mkuu wa taasisi hiyo.”

Kampuni ya ETG -Export Trading ndiyo ilipewa zabuni ya kuagiza na kusambaza kiuatilifu aina ya falcon sulphur dust kwa ajili ya korosho mwaka huu.

“Serikali ndiyo inaamua nani apime kama upimaji hauridhishi. Ndiyo maana tulimpelekea Mkemia Mkuu wa Serikali. Unajua haya ni mambo ya biashara yana ushindani mwingi. Kama Mkemia Mkuu amepima, unataka nani tena apime?”

Kaimu mkurugenzi wa Bodi ya Korosho (CBT), Hassan Jarufu alisema mzozo wa salfa hiyo ulitokana na kipimo cha Mesh ambacho watafiti wa TPRI walitaka kifikie 150 wakati salfa hiyo ilikuwa na kipimo cha 325 na ndicho kilikuwa kimekubaliwa kwenye mkataba kati yake na kampuni ya ETG.

Alisema kipimo hicho kimekuwa kikitumika katika misimu iliyopita na kilikuwa kikipitishwa na TPRI.

“Sasa walipokwenda kupima TPRI Arusha walitaka Mesh 150, tukajiuliza wameipata wapi hiyo? Yaani ni sawa na mimi nimeagiza gari aina ya Corolla ikafika, namwambia fundi wangu akaicheki, halafu aje aniambie hiyo gari si nzuri, labda ungenunua Carina,” alisema Jarufu.

Hata hivyo, Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samuel Manyele alisema salfa hiyo bado iko kwenye uchunguzi wa kimaabara, hivyo hawezi kuizungumzia.

Alipoulizwa sababu za kuruhusu itumiwe na wakulima wakati bado inachunguzwa, alisema: “Hilo ni suala la kimaabara, hatuwezi kukwambia lolote. Kama imekwenda kutumiwa na wakulima, siwezi kukujibu. Waulize walioruhusu.”

Ofisa uhusiano wa EGT, Fatuma Ali alisema kwamba kabla ya kuagizwa, walipeleka sampuli ya salfa hiyo TPRI.

Fatuma alisema kampuni hiyo imekuwa ikiagiza salfa na pembejeo nyingine kwa zaidi ya miaka 10 na ina masilahi na korosho, hivyo haiwezi kuagiza isiyo na kiwango.

Mbali na kauli hizo, baadhi ya watafiti ambao hawakuwa tayari kutajwa majina gazetini wameshauri kuundwa chombo huru cha wataalamu kuchunguza sababu ya taasisi hizo mbili kutoa taarifa tofauti za salfa hiyo.

Juni 10, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema salfa iliyoingizwa nchini kwenye makontena 211 haina kasoro na inafaa kwa matumizi ya kupulizia kwenye mikorosho.

Alitoa kauli hiyo alipozungumza na wajumbe wa kamati maalumu, waagizaji wa salfa na baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Korosho (CBT) kwenye kikao alichokiitisha kwenye makazi yake Oysterbay jijini Dar es Salaam.

“Bodi kaandaeni utaratibu wa kawaida kusambaza salfa kwa wakulima ili waanze kupuliza dawa hiyo. Wasichelewe kupuliza kwa sababu msimu umeshaanza,” alisema.

Juni 4, Waziri Mkuu alimuagiza Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samuel Manyele aende kuchunguza mzigo wa salfa uliokuwa Bandari ya Dar es Salaam baada ya kutokea mkanganyiko uliosababishwa na ripoti ya TPRI kuwa salfa hiyo haikidhi viwango.

-->