Watafiti wazindua programu ya kupanga maeneo kwa simu

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ardhi na Mtafiti Mshiriki wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF), Yvonne Matinyi akionesha kitabu cha maelekezo ya programu ya Lotizer iliyozinduliwa Dar es Salaam, jana. Kulia ni Profesa Fortunata Songora na Profesa Haidari Amani walioshiriki katika utafiti wa upimaji ardhi. Picha na Elias Msuya

Muktasari:

Wasema hawaingilii kazi za Serikali, bali wanawawezesha wananchi kuepusha migogoro

Dar es Salaam. Wakati Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ikieleza kuwa asilimia 70 ya makazi jijini hapa ni holela, taasisi mbili za utafiti zimezindua programu ya simu kwa ajili ya kupanga maeneo mapya.

Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF) na nyingine ya Grade kutoka Lima nchini Peru, zilizindua programu hiyo jana inayoitwa Lotizer.

Programu hiyo (app) imezinduliwa kutokana na utafiti wa ‘Upangaji wa hiari wa makazi katika jamii’ uliofanywa na taasisi hizo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Machapisho wa ESRF, Profesa Fortunate Songora alisema utafiti huo umebaini changamoto nyingi kwa wananchi wanaoishi katika makazi holela.

“Kuwapo kwa makazi holela kumeleta uhasama baina ya majirani, kutokana na magari ya zimamoto kutofika maeneo husika kwa wakati, wagonjwa kushindwa kufikishwa maeneo ya huduma na watoto kukosa maeneo ya kuchezea,” alisema Profesa Songora.

Akieleza kuhusu programu hiyo, Jire Tunguhole ambaye ni mtafiti wa ESRF, alisema inapatikana bure kwa wananchi kwa kutumia simu za mkononi na wakishaipakua wanaweza kujipangia maeneo yao.

“Programu hii itawasaidia wauzaji na wanunuzi wa viwanja kupanga maeneo ili wanunuzi wasiingiliane na kusababisha migogoro,” alisema Jire.

Hata hivyo, Jire alisema programu hiyo haihusishi upimaji wa ardhi kwa ajili ya kutoa hati, akisisitiza kuwa lazima kwenda idara ya ardhi kwa ajili ya kupima kupata hati.

“Sisi hatuingilii kazi za Serikali, bali tunawawezesha wananchi kupanga maeneo yao ili kuepusha migogoro ya viwanja na kutoa nafasi ya kutosha kwa makazi na huduma zingine muhimu,” alisema Tunguhole.

Baadhi ya madalali na viongozi wa mitaa kutoka sehemu mbalimbali za Dar es Salaam waliilaumu Serikali kwa kuchelewa kupima maeneo na kusababisha uvamizi na baadaye kuwabomolea nyumba wananchi wanaouziwa.

Profesa Haidari Amani wa ESRF alisema wanafanya kazi kwa kushirikiana na Serikali za mitaa, ambazo hutambua watu wanaouza na kununua viwanja.

“Tunafanya kazi na Serikali za mitaa, maana watu wanaponunua viwanja huenda kupata utambulisho. Lengo ni kuhakikisha kuwa eneo linalopimwa halijapangiwa kazi nyingine na Serikali,” alisema.

Alisema programu hiyo itasaidia wananchi kuepuka migogoro ya ardhi kwa kuuziana viwanja holela.