Watano washikiliwa sakata la kuunganisha bomba la mafuta

Muktasari:

Kilanglani anadaiwa kujichotea mafuta kutoka katika bomba hilo alilolipitisha chini ya ardhi.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limewakamata watu watano, akiwemo mwalimu wa Shule ya Msingi ya Kisiwani Kigamboni, Lebeka Nganji kwa kujihusisha na uuzaji wa mafuta ya dizeli yanayosadikiwa yalitoka katika bomba lililounganishwa kwa wizi.

Inadaiwa kuwa bomba hilo liliunganishwa na Samwel Kilanglani (63), ambaye nyumba yake iko umbali wa takribani mita 20 kutoka lilipo bomba kuu la mafuta la Tanzania na Zambia (Tazama).

Kilanglani anadaiwa kujichotea mafuta kutoka katika bomba hilo alilolipitisha chini ya ardhi.

Imedaiwa kwamba mfanyakazi huyo mstaaafu wa Tazama alianza kutoboa bomba la kwanza na kukuta lina mafuta ghafi na kuliziba, kisha kutoboa jingine lililokuwa na dizeli na kujiunganishia hadi nyumbani kwake.

Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Benedict Kitalika aliwataja watuhumiwa wengine kuwa ni Bariki Dickson, Christon Kapinga na Farhan Ahmed ambao wote wanaishi Kigamboni.

Alisema kukamatwa kwa watuhumiwa hao kunatokana na Kilanglani kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kuwataja wenzake ambao huchukua na kuuza mafuta hayo.

“Huyu mtuhumiwa alisema hayupo peke yake hivyo ana wenzake wanashirikiana dili hilo, ndiyo akawataja hao wanne akiwemo mwalimu wa Shule ya Msingi Kisiwani,” alisema.

“Tuliwakamata watuhumiwa sehemu mbalimbali za Kigamboni ambao wote wanafanya dili hilo la kunyonya na kuuza mafuta ya dizeli kutoka kwenye bomba kuu,” alisema Kitalika.

Juzi mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa alieleza kuwa Kilanglani alibainika baada ya mafuta yaliyokuwa yanavuja kuanza kusambaa barabarani.

Mgandilwa alisema Januari 6, walipelekewa taarifa kuwa mafuta yamesambaa kwenye njia ya mabomba ya Tazama yanayopita Tungi, Kigamboni.

Alisema baada ya kupewa taarifa hizo walienda hadi eneo hilo na kuamua kuchimba ili kubaini tatizo.

“Awali tulihisi bomba kubwa limepasuka. Tuliamua kuchimba ili kuyakabili mafuta yasiweze tena kuvuja na kuwasababishia athari wananchi,” alisema.

Alisema wakati wakiendelea na kazi hiyo, walikuta mabomba makubwa matatu ya mafuta, mawili yalikuwa yametobolewa; moja likipitisha mafuta ghafi ambalo lilionekana kuwa limezibwa.

“Bomba jingine ambalo lilikuwa la mafuta ya dizeli lilikuwa limeunganishwa kwa chini ya bomba jingine dogo kwa kutumia koki, tulivyofuatilia tukabaini limeelekea nyumbani kwa Kilanglani,” alisema.

“Huyu mtuhumiwa ni mtaalamu sana. Mtu mtu wa kawaida hawezi kuunganisha chini kwa chini, ndiyo maana alipogundua bomba la kwanza linatoa mafuta machafu akaziba na kutoboa jingine lililokuwa na mafuta ya dizeli.

“Mafuta yanaposhushwa kwenye meli hupita katika mabomba kwa kusukumwa na mashine kuelekea kituo cha kuhifadhia cha Tazama. Mabomba hayo yamepita karibu na nyumba yake.”