Watanzania, Wanigeria wanaswa na dawa za kulevya

Muktasari:

Akizungumza na waandishi wa habari jana saa nne usiku makao makuu ya Uhamiaji, Kaimu Kamishna wa Usimamizi na Udhibiti wa Mipaka, Kagimbo Hoseah alisema watuhumiwa walikamatiwa eneo la Masaki jijini Dar es Salaam.

Idara ya Uhamiaji imewakamata Watanzania watatu na raia watano wa Nigeria wakiwa na dawa za kulevya zikiwamo Heroin, Cocaine, bangi na mashine ya kuzitengeneza dawa hizo

Akizungumza na waandishi wa habari jana saa nne usiku makao makuu ya Uhamiaji, Kaimu Kamishna wa Usimamizi na Udhibiti wa Mipaka, Kagimbo Hoseah alisema watuhumiwa walikamatiwa eneo la Masaki jijini Dar es Salaam.

Hoseah aliwataja Watanzania kuwa ni Ruth Kabezi, Lucy Adolf na Lizzy Minja ambaye ni wakili wa kampuni mmoja ya uwakili.

Raia wa Nigeria ni Bisola Adeyemi, Olasunkanmi Kayode, Aaron Ejeh, Obina Nwauba na Darlington Nwauba ambaye ni mhitimu wa Shahada ya Sayansi ya Kompyuta (Computer Science) kutoka Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala tawi la Tanzania .

“Tunaendelea na uchunguzi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi, tutakapokamilisha hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa ikiwamo kuwafikisha mahakamani,” alisema Hoseah.

Alisema watu hao ni hatari kwa usalama wa Taifa kutokana na biashara wanayojihusisha nayo.

Hoseah amewaomba Watanzania kutoa ushirikiano wanapobaini watu wanaojihusisha na uhalifu.