Watanzania kuingia bure hifadhi za Taifa

Muktasari:

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amesema fursa hiyo itaanza Juni 2 hadi 4.

Dar es Salaam. Watanzania wamepewa fursa ya kuingia bure kwenye hifadhi za Taifa kwa siku tatu katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amesema fursa hiyo itaanza Juni 2 hadi 4.

Akizungumzia jana maadhimisho hayo ambayo huadhimishwa Juni 5 ya kila mwaka, Makamba alisema kitaifa yatafanyika Kijiji cha Butiama mkoani Mara.

Alisema fursa hiyo inalenga kuwawezesha wananchi kujionea wanyama kwenye hifadhi ambao wapo kutokana na utunzaji wa mazingira. “Kama unaishi maeneo ya karibu na hifadhi unaweza kwenda Arusha, Serengeti, Ngorongoro, Ruaha, Katavi, Saadani, Mikumi na kwingineko,” alisema January.

Alisema wameamua maadhimisho hayo yafanyike Butiama kuanzia Juni Mosi hadi 4 ili kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyekuwa mwanamazingira namba moja nchini.

Alisema watamuenzi kwa kukumbuka mchango wake katika uhifadhi wa mazingira na kwamba, bila msimamo wake Taifa lisingekuwa linasifika kwa uzuri na vivutio vyake.