Watanzania wadaiwa kuzikalia fursa za kilimo

Muktasari:

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Saggot, Geoffrey Kirenga aliyasema hayo mwishoni mwa wiki.

Dar es Salaam. Kituo cha Mpango wa Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (Saggot), kimetoa rai kwa vyombo vya habari kuwa mstari wa mbele kuhamasisha kilimo na kuzitangaza fursa zake.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Saggot, Geoffrey Kirenga aliyasema hayo mwishoni mwa wiki.

Alisema katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Tanzania ina fursa nyingi za kilimo lakini hazijafikiwa au kuchangamkiwa na wakulima kutokana na kukosa uthubutu na taarifa za uhakika.

“Ili kulikoa hili, wanahabari wanayo nafasi nzuri ya kuzitangaza fursa hizi ili sekta ya kilimo iweze kukua na kuinua kipato cha wakulima wadogo na wakubwa,” alisema Kirenga.

Alisema sekta ya kilimo inazo fursa nyingi kwa maendeleo ya Watanzania, wanahabari wakiziandika na kuzitangaza mara kwa mara, wengi watahamasika na kujikita katika shughuli hiyo. Akitolea mfano kiwanda cha kukoboa mpunga kilichopo Kilombero, alisema ni cha kwanza kwa ukubwa na ubora katika ukanda wa Afrika Mashariki lakini hakizalishi mpunga wa kutosha.

“Mfano mwingine ni kiwanda cha maziwa cha Asas kinachoongoza kwa usindikaji maziwa katika ukanda huu. Kwa siku kina uwezo wa kusindika lita 50,000 lakini wanapata lita 20,000 kutoka kwa wafugaji,” alisema Kirenga.

Alisema hizo ni fursa zinazopotea kwa madai kuwa ng’ombe waliopo hawana malisho bora.

“Lakini cha kushangaza, Australia wanatumia nyasi za Tanzania kulisha ng’ombe wao halafu wanakuja kutuuzia nyama na maziwa,” alisema.

Alisema, “Vilevile tuna tatizo la kuhifadhi chakula, mahindi yanayozalishwa nchini kwa mwaka ni kati ya tani milioni 6 hadi 7, lakini yanayohifadhiwa kwa njia za kisasa ni kati ya tani milioni moja hadi mbili, yaliyobaki yanahifadhiwa kwa njia za kienyeji, yanaishia kuharibika, ipo haja kwa Serikali ikatengeneza maghala katika maeneo ya uzalishaji.”

Akizungumzia malengo ya kuanzishwa kwa mpango huo, Naibu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Saggot, Jennifer Baarn alisema; “kazi yetu ni kuangalia matatizo yanayorudisha nyuma sekta ya kilimo na namna ya kuyatatua ili kuhakikisha mnyororo wa kuongeza thamani ya mazao unaleta tija kwa wakulima, hasa wadogo.”